33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Askofu Ruwa’ichi ahamishiwa wodi ya kawaida

Avelina Kitomary -Dar es salaam

ASKOFU Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Ruwa’ichi,  amehamishiwa wodi za wagonjwa wa kawaida baada ya afya yake kuendelea kuimarika.

Akitoa taarifa hiyo jana Dar es Salaam, Ofisa Habari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (Moi), Patrick Mvungi, alisema jopo la wataalamu saba wanaomhudumia askofu huyo, limeamua kumuhamisha kutoka katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU), baada ya kujiridhisha na maendeleo ya afya yake.

“Jopo hilo limefanya maamuzi hayo leo (jana) saa mbili asubuhi baada ya kufanya tathmini ya vipimo pamoja na taarifa mbalimbali za maendeleo ya askofu toka alivyopelekwa na kufanyiwa upasuaji,” alisema Mvungi.

 Alisema kuwa jopo hilo la wataalamu wa afya ilihusisha vitengo mbalimbali katika taasisi hiyo ili kuhakikisha askofu anarejea katika hali yake ya kawaida.

“Kuna madaktari bingwa wa upasuaji wa ubongo (Neurosurgeon), madaktari bingwa wa usingizi (Anaesthesiologist), magonjwa ya ndani (Physician), wataalamu wa lishe (Nutritionist), wauguzi wabobezi (Specialised Nurse) pamoja na wataalamu wa mazoezi ya tiba (Physiotherapist),” alifafanua Mvungi.

Aidha aliwataka Watanzania hususani waumini wa Kanisa la Katoliki kutokuwa na wasiwasi badala yake wamuuombee ili arejee kwenye majukumu.

Askofu Ruwa’ichi alifikishwa Moi Septemba 9, mwaka huu saa tano usiku  akitokea katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi.

Baada ya kupolewa, wataalamu wa Moi walimfanyia uchunguzi na vipimo na kubaini alihitaji upasuaji wa dharura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles