DUBLIN, IRELAND
OFISA wa zamani mwandamizi katika Makao Makuu ya Kanisa la Katoliki duniani, Vatican, amemtaka Kiongozi wa Kanisa hilo duniani, Papa Francis, kujiuzulu kwa vile alifahamu na kufumbia macho tuhuma za udhalilishaji ngono zilizomkabili kardinali wa zamani Marekani.
Hiyo ni mara ya kwanza kwa ofisa wa juu ndani ya Kanisa kumlenga Papa Francis katika mlolongo wa kashfa zinazolikumba kanisa hilo tangu kufichuliwa  tuhuma za ngono dhidi ya makasisi miaka ya mwanzo ya 2000.
Katika taarifa yenye kurasa 11 kwa vyombo vya habari vya Kanisa hilo wakati wa ziara ya Papa nchini Ireland, Askofu Mkuu Carlo Maria Vigano alituhumu orodha ndefu ya maofisa wa Vatican na Marekani kuficha kashfa zilizomkabili Kardinali Theodore McCarrick, aliyejiuzulu kwa aibu mwezi uliopita.
“Papa Francis amekuwa akisisitiza uwazi katika Kanisa,” aliandika Vigano, ambaye si mara ya kwanza kumkosoa Papa.
“Katika kipindi hiki, anatakiwa kukiri makosa yake na kuendana na misingi ya kutovumilia kabisa kashfa za aina hiyo.
“Papa Francis anatakiwa kuwa wa kwanza kuwa mfano kwa makardinali na maaskofu walioficha uchafu wa McCarrick na ajiuzulu pamoja nao wote,” alisema.
Maofisa wa Vatican walishindwa kutoa kauli yoyote mara moja kuhusu taarifa hiyo iliyochapishwa katika gazeti la National Catholic na mengine mengi ya kihafidhina nchini Marekani na Italia.
Vigano alisema Juni 2013 alimjulisha Francis baada ya kuchaguliwa na makardinali wenzake kuwa papa kuhusu tuhuma zinazomkabili McCarrick.
Vigano alikuwa mwakilishi wa papa mjini Washington kuanzia mwaka 2011 hadi 2016.
Alisema pia kuwa aliwafahamisha maofisa waandamizi wa Vatican mapema 2006 kuwa McCarrick anashukiwa kuwadhalilisha wanaseminari wakati akiwa askofu wa dayosisi mbili za New Jersey kati ya mwaka 1981 na 2001. Alisema kamwe hakupokea majibu ya taarifa yake hiyo.
Pia alimtuhumu mrithi wa McCarrick wa uaskofu mkuu wa Washington, Kardinali Donald Wuerl kufahamu tuhuma hizo. Hata hivyo, Wuerl amesisitiza kutozifahamu.
Taarifa hiyo ni pigo jingine juu ya uhalali wa Kanisa nchini Marekani baada ya wiki mbili zilizopita Mahakama ya Pennsylvania kutoa matokeo ya uchunguzi ambao ulibainisha kuwa mapadri 301 jimboni humo waliwalaghai kwa ngono wavulana  miaka 70 iliyopita.
Julai mwaka huu, McCarrick alikuwa kardinali wa kwanza aliye kazini kujiuzulu wadhifa wake baada ya uchunguzi kubainisha alimdhalilisha mvulana wa miaka 16.