WAZIRI MAKAMBA KUFUNGUA MKUTANO WA KIMATAIFA

0
958

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, anatarajia kufungua mkutano mkubwa  wa kimataifa unaohusu matumizi ya programu huria kwa usimamizi wa mazingira jijini Dar es Salaam kesho.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Usimamizi  wa Mazingira nchini (NEMC), Dk. Vedast Makota, mkutano huo muhimu unawakutanisha wataalamu kutoka pande zote za dunia na kuweza kubadilishana uzoefu na kuhimiza matumizi ya teknolojia.

“Mkutano huu unawaleta washiriki  zaidi ya 600 ambao wamebobea katika masuala ya mazingira na matumizi bora ya teknolojia,” alisema Dk. Makota na kuongeza kuwa  mkutano huo una faida nyingi kwa Tanzania kama nchi.

Alisema mkutano huo unalenga pia kuhakikisha kuwa mataifa bila kujali uwezo wake yanakwenda sambamba na matumizi ya teknolojia kwa usimamizi endelevu wa mazingira.

“Mkutano huu utasaidia sana kwa washiriki kufahamu mbinu na njia mbalimbali zinazotumiwa katika kulinganisha rasilimali mazingira na maendeleo ya kuchumi,” alisema.

Alisema mkutano huo mbali na mambo mengine, utasaidia kuimarisha uwezo wa Tanzania  kama mwenyeji wa mkutano huo kwenda sambamba na matumizi bora na endelevu ya mazingira kwa ustawi wa watu wake.

“Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi kubwa sana duniani na pia kama kiungo cha ubunifu na majaribio,” alisisitiza.

Dk. Makota alisema Tanzania  ipo mstari wa mbele katika kuwawezesha wananchi wake masuala ya kijiografia na hivyo kuwa na  sifa  stahiki za kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa unafahamika kama  FOSSG4.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here