WACHUNGAJI, wahudumu na walei wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN), wamemshauri Askofu Boniphace Kwangu, kujiuzulu baada ya kudaiwa kukiuka katiba na kuwasimamisha wenzake bila kufuata utaratibu.
Ushauri huo umekuja baada ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa kuchunguza tuhuma zinazomkabili Kwangu kuwasilishwa na kupendekeza mbele ya Askofu Mkuu Msaidizi wa Kanisa la Anglikana hapa nchini, Oscar Mnung’a, kuwa anapaswa aache kuwafukuza wenzake kwa kutumia polisi wakati majadiliano ya hali na hatima ya mgogoro wao uliodumu kwa muda mrefu ndani ya dayosisi hiyo bado yanaendelea.
Awali, akisoma taarifa hiyo mbele ya Mnung’a, Katibu Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Askofu Johnson Chinyong’ole, alisema ni kweli kamati hiyo ilithibitisha kumkuta Kwangu na makosa mbalimbali ikiwamo kumsikiliza zaidi mkewe kuliko ushauri wa wazee na wachungaji, kutumia vibaya na kuuza mali za kanisa na kuwasimamisha wachungaji 19 bila kuwasikiliza huku chanzo cha mgogoro huo kinatajwa kuwa ni uroho wa madaraka wa askofu, tamaa ya fedha na kushindwa kutekeleza vikao vya dayosisi hiyo.
“Kamati hii pia ilibaini kuwa askofu wetu amekuwa akikiuka katiba kwa kupanga na kuchagua wahudumu wa kanisa, kuingilia mambo ya kanisa kuu na alichonga sanduku la sadaka na kufuli analo mwenyewe na wakati mwingine huingia kanisani bila kuvaa vazi la kiaskofu, hali hii inasababisha wachungaji kugawanyika katika makundi manne likiwamo linalomuunga mkono na linalompinga askofu,” alisema Chinyong’ole.
Ripoti hiyo pia ilimkuta Kwangu na makosa ya kwenda kinyume na utaratibu wa fedha ikiwamo kutorudisha taarifa za matumizi ya fedha na ukiukwaji wa taratibu za sadaka hali inayosababisha uhusiano kati yake na wachungaji kudorora kutokana na kitendo cha kutumia lugha isiyofaa kwa kuwaita wachungaji hao kuwa ni wajinga na hawajui kutafuta fedha.
Pia ilipendekeza Kwangu apewe onyo ama karipio la haraka kwa kuwa dayosisi hiyo ina hali mbaya kiuchumi, kiuhusiano na kiuendeshaji hivyo ni muhimu kwa askofu huyo kuelimishwa ili ajue namna ya kuiongoza kwa kuwa kufukuzwa huenda lisiwe suluhisho la kudumu na likaibua migogoro zaidi kutokana na ukweli kuwa amezidiwa nguvu na makundi yaliyomuasi.
Baada ya kusomwa kwa taarifa hiyo, wachungaji walimtaka Kwangu kujitathmini na kung’atuka kwa hiari yake ili kunusuru heshima ya kanisa hilo kuliko kuendelea kung’ang’ania, kuligawa na kuharibu heshima ya nyumba ya maaskofu wa Anglikana.
“Hata kama wengine watakubali abaki, mimi sitakubali, ni lazima mmoja wetu atupwe baharini na mnapokwenda huko hakikisheni majibu ya askofu kupumzika mnayaleta mapema maana mkichelewa mtaleta mambo mengine, sisi hatupigi tena maaskofu lakini msipochukua hatua za haraka mtaleta shida, apumzike haraka kabla hajatuletea shida,” alipendekeza Mchungaji Joseph Samwel.
Naye Mchungaji Daniel Kuboyoka, alisema ni lazima ofisi (askofu mkuu) iweze kumstaafisha Kwangu kutokana na uwezo mdogo wa kuongozi alionao ili kulinusuru kanisa maana limedhalilika vya kutosha na amefanya mengi ya kutosha hivyo ni bora ajiuzulu na dayosisi ikae miaka mitano bila askofu ili itulie kuliko kuiacha ilivyo.
Kwa muda mrefu dayosisi hiyo imegubikwa na migogoro mingi ikiwamo matukio ya wachungaji kuwakaba, kuwapiga na kuwazuia maaskofu wenzao kuingia kanisani na kutofautiana kati ya askofu na wachungaji kuhusu mali na migogoro iliyosababisha viongozi hao kuitwa mara kwa mara kwa kusuluhishwa na kujieleza ni kwanini dayosisi hiyo isifutwe.