Na Mwandishi Wetu, Pwani
Askari wa Jeshi la Polisi aliyekuwa anafanya kazi katika kituo cha Polisi Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani namba E 6472 Yusuph Said (52) amekutwa amejinyonga hadi kufariki dunia katika nyumba yake anayoijenga katika maeneo ya Miembe Saba kata ya Kongowe wilaya ya Kibaha.
Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba lilitokea Januari 18, saa 12 jioni maeneo ya Mibembe Saba B Wilayani Kibaha.
Kamanda Wankyo amesema Yusuph alikuwa akitumikia katika kituo cha Kibaha Picha ya Ndege, lakini siku ta tukio alienda Kongowe eneo ambalo alikuwa akiendelea na ujenzi wa nyumba yake na ndiko alikokutwa amefariki dunia kwa kujinyonga na kamba.
Aidha, Kamanda Nyigesa amesema amebainisha kuwa uchunguzi kuhusu tukio hilo bado unaendelea wakati taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu zikiendelea.
“Uchunguzi kuhusu tukio hili unaendelea wakati taratibu za kumsafirisha marehemu kwenda kwao Lindi kwa maziko zikiendelea,” amesema Kamanda Nyigesa.
Msaidizi wa Balozi wa Nyumba kumi kwenye eneo hilo, Imelda Kitosi, akisimulia tukio hilo amesema akiwa nyumbani alipigiwa simu kuwa kuna tukio la mtu kijinyonga ndipo akaenda kushuhudia akiwa na baadhi ya majini zake.
Imelda amesema alipofika alielezwa na wazazi wa watoto waliokuwa karibu ya eneo hilo kuwa kuna watoto waliokuwa wanacheza kombolela nje ya nyumba hiyo ambao walisema walisikia mtu anajipiga ndani ya nyumba na walipochungulia wakamkuta tayari yupo chini akiwa na kamba shingoni na walikimbia kwenda kutoa taarifa.
Wazazi hao walipofika katika nyumba hiyo ambayo bado inajengwa walimkuta askari huyo tayari ameshafariki ndipo walipoanza kutoa taarifa kwa viongozi na kumpigia msaidizi huyo wa balozi.
“Mimi sasa baada ya kupigiwa simu niliingia hapa pamoja na baadhi ya watu waliokuwa karibu tulimkuta yuko kwenye chumba ambacho kilikua kinajengwa kama bafu au choo kamba kaifunga juu na chini kulikuwa na tofali ambalo baada ya kuhangaika sana mguu mmoja tulikuta kama umepiga goti na mwingine umeegemea tofali huku kamba ikiwa shingoni.
“Baada ya kushuhudia tukio hilo ndipo tukapiga simu Polisi kutoa taarifa na walifika na kuchukua mwili wa marehemu,”amesema.