Na Nyemo Malecela-Kagera
ASKARI wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Denis Minja, amejitolea kumlea mtoto huyo wa mwaka mmoja na miezi sita ambaye Mei 21 mwaka huu alimuokoa katika shimo la choo cha Shule ya Msingi ya Murgwanza iliyoko wilayani Ngara mkoani Kagera
Minja ametangaza nia yake ya kumlea mtoto huyo jana baada ya kuvalishwa cheo cha ukoplo alichotunukiwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, John Masunga, kutokana na kitendo cha ujasiri cha kuokoa maisha ya mtoto huyo.
Minja alisema tayari ameanza taratibu za kisheria katika idara ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Ngara ili mtoto huyo akitoka hospitali aweze kuishi naye.
“Mbali na mtoto huyo, mimi na mke wangu tuna watoto wawili, wa kwanza ana miaka tisa na wa pili ana miaka miwili na miezi mitatu.
“Mimi ni mzazi na nina watoto, kwa hiyo kitendo cha kuchungulia kwenye shimo na kumuona mtoto analia sana, niliniumiza ndio niliamua kujitoa muhanga kwani wananchi waliokuwa wameshikilia kamba niliyojifunga kiunoni walikuwa waamuzi wa maisha yangu,” alisema Minja.
Alisema kama wananchi hao wangeiachia kamba aliyokuwa amejifunga kiunoni wakati anaingia kwenye shimo kumuokoa mtoto huyo, angeweza kupoteza maisha.
Minja alisema shimo ambalo mtoto huyo alitumbukizwa lina urefu wa futi 30, lilikuwa na giza na alivyoingia aligundua mtoto alikuwa amefungwa kanga mdomoni hivyo alianza kumpatia huduma ya kwanza humo humo shimoni.
Alisema huduma hiyo ni pamoja na kumuondoa uchafu (kinyesi) uliokuwa umemuingia mdomoni na puani ili aweze kupumua na baada ya kumsafisha alimkumbatia kifuani mwake na kuanza kuwapa maelekezo wananchi waliokuwa nje ya shimo ili waweze kumvuta na atoke katika shimo na mtoto.
Alisema kilichomsaidia mtoto huyo hasipoteze maisha katika shimo hilo ni mbao zilizokuwa zimewekwa katika shimo hilo kwa ajili ya kukanyagia wakati wanafanya ujenzi.
alisema kutokana na mbao hizo, mtoto huyo alivyotupwa kwenye shimo hilo hakwenda chini moja kwa moja bali alikuwa akiangukia kwenye mbao hizo hadi alivyofika mahali akagota.
“Kwa hiyo nilimkuta amelalia baadhi ya mbao kwenye kinyesi na baada ya kumtoa kwenye shimo hilo tuligundua alikuwa na njaa hivyo tulimpatia maziwa na madaktari walimuwekea dripu ya glucose ili apate nguvu.
“Na jana mtoto huyo alifanyiwa upasuaji ili kurekebisha mguu wake uliovunjika wakati alipotupwa kwenye shimo hilo,” alieleza.
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi hilo mkoani Kagera, Inspekta Hamis Dawa, alisema kitendo kilichofanywa na askari huyo ni cha ujasiri kwani alihatarisha maisha yake kwa ajili ya kupigania uhai wa binadamu mwingine.
“Tayari tumemvalisha cheo Cha ukoplo askari ZM 3847 Fire Kostabo na sasa atakuwa ZM 3847 Koplo, tunawaomba askari wengine kuiga mfano huu kwa kuendelea kujitolea maisha yao kwa ajili ya wengine kwa kutumia vifaa vitakavyokuwepo katika mazingira yanapotokea matukio,” alisema.
Alisema wakati Minja anafanya uokoaji kwa mtoto huyo hakuwa na kifaa chochote cha kumlinda isipokuwa kamba aliyojifunga kiunoni ili kuingia kwenye shimo hilo la choo.