Na AVELINE KITOMARY – DAR ES SALAAM
SAFI wa vyoo ni muhimu kulinda afya ya binadamu na kuweka mazingira salama ambayo yanafanya jamii iweze kuepukana na magonjwa ya lipuko.
Wapo watu ambao wanajihusisha kufanya kazi za usafi wa vyoo ‘maarufu kama vyura’ ikiwemo kuzi- bua vyoo vilivyoziba na kuhamisha majitaka kwa vyoo vilivyojaa.
Kazi hiyo ina umuhimu mkubwa kwa jamii na uwezekano wa vijana kupata ajira ni mkubwa kwani baada ya uzoaji wa majitaka pia yanaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali kama mbolea, gesi na umwagiliaji.
Ingawa kazi hii ni muhimu lakini pia ni hatarishi hasa kwa wale wanaofanya bila kuwa na vitendea kazi sahihi.
Wapo wafanyakazi wanaopoteza maisha au hata kujeruhiwa kutokana na mazingira mabaya ya utendaji kazi.
HALI ILIVYO
Ripoti zilizotolewa hivi karibuni na Shirika la Wateraid kwa kush- irikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Benki ya Dunia, zinasema pamoja na kuimarika kwa huduma za jamii katika nchi zinazoendelea, bado wafanyakazi wa usafi vyooni wako hatarini kuathirika kiafya.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa India pekee kati ya mwaka 2017 na 2018 watu watatu wanaofanya kazi hiyo hufariki dunia kila baada ya siku tano, huku kwa mwezi mmoja watu 18 wanapoteza maisha na kwa mwaka ni watu 216.
Shirika la Water Aid Tanzania limesema watu wanaojihusisha na kazi za usafi vyooni wako hatarini zaidi kupoteza maisha kutokana na mazingira hatarishi.
Meneja Miradi Mwandamizi wa Water Aid Tanzania, Twaha Mubarak, anasema kuna haja ya kuwaangalia wafanyakazi wa vyooni kwani wao ndiyo wanahakikisha jamii inakuwa katika mazingira salama kwa kufanya usafi.
Anatoa wito kwa Serikali kuten- geneza mazingira wezeshi na mfumo rasmi kwa watu wanaofanya kazi za usafi wa uzoaji taka wa vyoo.
“Katika suala la usafi, bado kuna watu hatujawatazama sawasawa, watu hawa ni wale wanaofanya kazi sekta ya usafi, hasa wale wanaohusika na uzoaji wa taka za vyooni hadi kutupa takataka.
“Ripoti inabainisha mazingira mabaya ya mamilioni ya wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika mazingira hatarishi kwa afya zao.
“Pamoja na kuimarika kwa huduma za jamii, kundi hili limekuwa likiach- wa katika mazingira mabaya, hawana vitendea kazi, lengo la ripoti ni kuinua ufahamu kuhusu mazingira hatarishi
wanayopitia watu hawa wa mnyor- oro wa usafi kama kusafisha vyoo, kutapisha mashimo ya vyoo, kusafisha mitaro na kusimamia njia ya kutibu maji taka.
“Wafanyakazi hawa mara kwa mara wanagusa vinyesi vya binadamu wakiwa hawana vifaa vya kuwakinga, hali hii inaweza kuwafanya kupata magonjwa hatarishi.
“Ukiacha vifo, kuna wale wa- naopata maumivu, ajali na magonjwa ya mara kwa mara au yanayojirudia na pia kuna ugonjwa kama kipindupindu ni hatari,” anasema Mubarak.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhai Mazingira na Watu (UMAWA), Mathias Milinga, anaiomba Seri- kali kuongeza nguvu katika kazi za uchakataji wa maji taka ili kuongeza ajira kwa vijana.
“Huwa tunakuwa na mfumo rasmi wa kuchakata na kufanya uzalishaji ambao utatumika kwa mahitaji ya bin- adamu, ipo mitambo ambayo inatu- mika, yale maji taka yanafaa kutengen- ezea mbolea, mkaa wa kupikia, gesi na pia maji masafi, kwa hiyo hii itasaidia kutunza mazingira,” anasema Milinga.
KISA CHA CHISENGO
Julius Chisengo ni mkazi wa jiji
la Dar es Salaam na baba wa watoto
watano, kwa miaka 12 sasa amekuwa
akifanya kazi za usafi vyooni kama
kuhamisha majitaka na kuzibua vyoo.
Kutokana na kukaa kazini muda mrefu uwezo wake wa kufanya kazi
hiyo sasa umekuwa mkubwa hata uelewa umeongezeka pia.
Anasema kazi hiyo ndiyo inayom- wingizia kipato na kulisha familia yake hivyo ni muhimu kwake.
“Nina muda mrefu tangu nianze kufanya kazi hii na naipenda kwa sababu inanisaidia. Nasomesha wa- toto, natunza familia hivyo nafaidika japo ni kazi hatarishi pia,”anasema.
Chisengo anasema kazi hiyo pia ilishawahi kumwathiri kiafya na kum- sababishia ulemavu wa mguu.
“Changamoto kubwa niliyoipata
nilivunjika mguu wa kulia wakati
ule ambao sina elimu, mtu akiniita
kuzibua choo naenda tu sasa siku hiyo
nilikanyaga mti uliooza ukavunjika
nikaanguka na kupata ulemavu.
“Niliuguzwa kwa muda mrefu hadi nilipopata nafuu, si unaona huu mguu wangu mmoja (anamuonesha mwandishi) haulingani na mwing- ine japo najitahidi kusimama vizuri. Huu ni kama ulemavu tu kwangu lakini hata sasa namshukuru Mungu,” anasema.
Anasema mazingira, kutokuwa na vitendea kazi na upeo mdogo wa ujuzi vilisababibisha akaumia.
“Kwasasa afadhali kuna tofauti ki- dogo uelewa ninao nimepata mafunzo mengi na ninapokwenda kazini naan- galia kwanza usalama na vitendea kazi nitakavyotumia,” anasema.
Anasema wafanyakazi wenzake wawili pia waliwahi kuumia na wote sasa wana ulemavu wa miguu.
“Hizi kazi zinahitaji vifaa, usipoku- wa na ujuzi kuumia ni rahisi kwa sababu kila kifaa kina sehemu yake.
“Wakati nafanya kazi kuna marafiki
zangu wawili walipata ajali na kuumia na sasa ni walemavu wa miguu,” anasema.
Chisengo anatoa wito kwa serikali
kuangalia kazi hizo kwani ni sehemu muhimu ya afya ya jamii.
“Tunafanya kazi ya kulinda afya ya jamii, sisi tunasaidia kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kama kipin- dupindu na mengine.
“Naomba Serikali watutengenezee mfumo rasmi na watoe elimu maeneo yote ili watu wajue kazi hii inahitaji nini,” anasema Chisengo.
MAJITAKA NI DHAHABU
Tekonlojia inaweza kubadilisha ma- jitaka hasa ya vyooni kwa matumizi mengine.
Meneja Miradi Ufuatiliaji Tathimini
na Ripoti kutoka Shirika la Wateraid,
Reginald Kwizela, anasema wana-
tumia majitaka kutengeneza maji
kwa ajili ya umwagiliaji na gesi kwa
matumizi ya nyumbani.
“Tukishachukua majitaka kutoka kwa mteja huwa tunayaleta kwenye kituo ambacho kina sehemu ya kum- waga.
“Unapomwaga pale maji yanain- gia kwenye shimo kubwa ambalo limejengwa kwa tofali halivuji na kuna sehemu yatakapofikia yanaha- mia upande wa chemba nyingine yanachujwa tope linabaki chini maji yanapanda juu.
“Unapomimina pale kuna bomba limeenda mpaka chini kwa hiyo maji yanahamia chemba ya pili, ya tatu zipo tisa sasa hiyo ya tisa ukioneshwa kuwa haya ni majitaka huwezi kuamini. Ni me- upe hayana hata harufu yakifika sehemu ya 10 yanaenda kwenye bwawa kwa ajili ya kumwagilia shamba.
“Gesi inatokana na tope kuna bomba limeenda moja kwa moja mpaka kwenye nyumba ya makazi, gesi hii inatumika kwa ajili ya kupikia,” anasema.
Anasema baada ya miezi mi- tatu tope likikauka huchukuliwa na kuwekwa sehemu nyingine tayari kutumika kama mbolea.