Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
UTAFITI wa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi nchini uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2014/15, umeibua mazito baada ya kubaini asilimia 71 ya Watanzania walio katika umri wa kufanya kazi hufanya shughuli za kustarehe, kulala na kujihudumia wenyewe.
Utafiti huo, unaonyesha vijana wenye umri wa miaka mitano na zaidi ambao wamekuwa wakifanya shughuli hizo kila siku, wakati wengine wakiwa kwenye shughuli za uchumi ambao ni asilimia 18.5, huku asilimia 10.6 ni shughuli za nyumbani zisizokuwa na malipo.
Pia unaonyesha kiwango cha watu wasiokuwa na shughuli za kiuchumi na hawataki kujishughulisha kimeongezeka kutoka asilimia 10.4 mwaka 2006/7 hadi 17.2 mwaka 2014/15.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya matokeo ya utafiti huo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa NBS, Dk. Albina Chuwa alisema hali hiyo ni changamoto kubwa kwa Taifa.
“Eneo hili ni muhimu kulitazama. Hii ni changamoto ambayo inatakiwa ifanyiwe kazi, lazima wanachi wabadili fikra zao wajiletea maendeleo bila ya kukaa na kusubiri mtu mwingine au Serikali iwaletee.
“Kwa upande wa wanawake, ingawa wanatumia muda mwingi kufanya shughuli za nyumbani bila malipo,ukipima utakuta wanachangia kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Muhagama alisema matokeo hayo yataisaidia Serikali kupanga sera za maendeleo.
“Inatisha kuona asilimia 71 wanafanya shughuli za kujihudumia wenyewe, kulala na kustarehe wakati wenzao wanajishughulisha kila siku kujenga uchumi, kweli hili ni eneo ambalo linapaswa kutupiwa macho.
“Imegeuka tabia ya baadhi ya Watanzania kukaa baa na kunywa pombe wakati wa saa za kazi, ndiyo maana hata Rais Dk. John Magufuli alipiga marufuku na huenda hawa ndiyo wanaoongoza kuilalamikia Serikali, ningefurahi tungepata takwimu hii. Imefika mahali lazima tubadilike tuseme hii ni aibu,” alisema.
Waziri Mhagama aliongeza. “Kwa mujibu wa utafiti huu mgawanyo wa ukosefu wa ajira maeneo mbalimbali ya nchi, unaonyesha Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia 21.5 ikifuatiwa na maeneo mengine ya mijini kwa asilimia 9.9 na vijijini 8.4.
Alisema jitihada zinahitajika upande wa walemavu ambako kiwango cha ukosefu wa ajira wenye umri wa miaka 15 na kuendelea mwaka 2014/15, ni asilimia 12.4 ambacho ni kikubwa zaidi ya kiwango cha kitaifa cha asilimia 10.3.
Awali akiwasilisha matokeo hayo wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Ajira na Bei wa NBS, Ruth Minja alisema utafiti huo ulizingatia viashiria 18 vinavyoshauriwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
“Utafiti unaonesha watu wenye uwezo wa kufanya kazi kuanzia umri wa miaka 15 ni milioni 25.7, wanaume ni milioni 12.4 na wanawake ni milioni 13.4 na kati ya hao nguvu kazi ya Taifa ilikuwa ni milioni 22.3 ambapo wanaume ni milioni 11.0 na wanawake ni milioni 11.2,’ alisema.