31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Asilimia 30 yazua sintofahamu upimaji viwanja Michese Dodoma

Na Ramadhan Hassan, Dodoma

Upimaji wa viwanja katika eneo la Michese jijini Dodoma umezua malalamiko kwa wananchi  wanaopimiwa viwanja hivyo huku wakihoji asilimia 30 wanayokatwa  na Kampuni ya upimaji ya GEO Plan imekuwa ikienda wapi.

Kutokana na hali hiyo Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru aliitisha Mkutano wa hadhara ambao uliwakutanisha wataalamu wa ardhi  kutoka Jiji la Dodoma, Kampuni inayopima eneo hilo ya GEO Plan, Kamati ya urasimishaji na  wakazi na wamiliki wa maeneo ya Michese.

Wakizungumza katika mkutano huo wakazi hao wamesema wanashangaa wakati wa zoezi la upimaji wa viwanja kwa wale wenye viwanja zaidi ya kimoja wamekuwa wakikatwa asilimia 30 hivyo wamehoji asilimia 30 hiyo inaenda wapi.

Mchungaji Nguvumali amesema kwamba wamekuwa wakiuliza maswali kuhusiana na hiyo asilimia 30 lakini hawapati majibu hali ambayo imekuwa ikiwapa wakati mgumu.

“Tunashukuru Mkurugenzi umekuja hapa kwetu tatizo kubwa kabisa ni hii asilimia 30 tunayokatwa katika viwanja vyetu inaenda wapi?, ukikutwa unaviwanja zaidi ya kimoja unakatwa asilimia 30 na ukiwa na viwanja vingi vinapunguzwa unapewa vichache,tunaomba majibu Mkurugenzi,”amesema.

Naye, Domestress Daud amesema kwamba Kampuni hiyo ya upimaji imekuwa ikiwakosesha usingizi kwani haiwashirikishi wananchi wakati wa upimaji kama mkataba wa awali unavyotaka.

“Wakati mwingine unasema afadhali ya CDA kuliko hawa wanaotupimia sasa hivi tunaomba mtusaidie,ardhi kwetu ndio kila kitu,”amesema.

Upande wake, Barbara Adory amesema kwamba wenye mashamba waachiwe wapimiwe halafu waachiwe walipe viwanja vyao wenyewe badala ya kuwekewa hiyo asilimia 30.

Akitoa ufafanuzi juu ya asilimia 30, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma,Mafuru amesema kwamba asilimia hizo zipo kisheria na ni kwa ajili ya  wale ambao viwanja vyao vimepitiwa na huduma za jamii kama vile shule,soko,barabara.

“Asilimia 30 zipo kisheria kila mtu hapa anaeneo sasa huyu aliyepitiwa na huduma za kijamii tumpeleke wapi, atapata hapa hapa kwa hizi asilimia 30 mtu mwenye viwanja 10 atatupa kadhaa ili na mwenzake apate,Jiji tunataka kila kitu kiende kwa haki na kila mmoja apate kiwanja hapa hapa Michese,”amesema Mafuru.

Kuhusiana na Kampuni ya upimaji ya GEO Plan,Mafuru amesema kwamba kuna Mamlaka ambazo zinasimamia makampuni ya upimaji hivyo kama itakutwa na makosa itawajibishwa mara moja.

Hata hivyo ametoa maagizo kwa Kampuni hiyo ya upimaji kubandika ramani katika eneo la wazi ili kila mmoja aweze kuona yupo katika eneo gani pamojana ramani za mipango miji.

“Pia nawapa wataalamu wangu nitawapanga kwa mitaa kwa siku 14 kupokea malalamiko,Jiji tunataka mambo yaende vizuri,”amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya upimaji ya GEO Plan,Silvan Magari,amesema kwamba Kampuni yake imefanya kazi kwa weledi katika eneo hilo ambapo amedai kwamba zaidi ya viwanja 6370 tayari vimeidhinishwa.

Naye, Afisa Ardhi wa Jiji la Dodoma,Aisha Masanja amesema kwamba Jiji la Dodoma limejipanga kuhakikisha eneo hilo linakaa vizuri kiramani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles