Mwandishi Wetu- Dar es Salaam
TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) tangu ilipoanzishwa mwaka 2015 hadi Aprili, mwaka huu, kati ya wagonjwa 334,774 iliyowatibu, asilimia 66 ya wagonjwa walikuwa na tatizo la ugonjwa wa shinikizo la juu la damu
Taarifa iliyolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Anna Nkinda Dar es Salaam jana, ilisema ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hutokea wakati nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa ya moyo kuwa kubwa kuliko kawaida.
Taarifa hiyo, ilisema jana Tanzania iliungana na mataifa mengine duniani kuazimisha siku ya shinikizo la juu la damu duniani.
“Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya kazi kupita kiasi ili kusukuma damu katika mishipa ya damu.
“Kwa kawaida ugonjwa wa shinikizo la damu halina dalili, ila likidumu kwa muda mrefu bila tiba lina madhara makubwa kiafya,”ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo, ilisema kuna aina mbili za ugonjwa wa shinikizo la juu la damu ambazo ni shinikizo la juu la damu la kurithi na shinikizo la damu linalosababishwa na magonjwa mbalimbali.
“Asilimia 95 ya wagonjwa wa shinikizo la juu la damu hawana sababu inayoweza kujulikana kisayansi.
“Ugonjwa wa shinikizo la juu la damu halina sababu inayoeleweka na mara nyingi inaweza kusababishwa na mgonjwa kuwa na historia ya ugonjwa katika familia yao, uzito mkubwa kupindukia, matumizi ya chumvi nyingi, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na umri mkubwa,”ilisema taarifa hiyo.
Asilimia kubwa ya watu wanaopata ugonjwa wa shinikizo la juu la damu huwa katika kundi hili na magonjwa mbalimbali kama figo, mishipa ya moyo na mfumo wa homoni. Aina hii ya shinikizo la juu la damu huathiri asilimia 5 ya wagonjwa wenye shinikizo.
Kwa mfano aina hii ya shinikizo la damu huweza kuwatokea kinamama wakati wa ujauzito na hupona mara baada ya kujifungua.
Taarifa hiyo, ilisema ugonjwa huo unaweza kusababisha mwili kupooza,kiharusi (stroke), shambulio la moyo (heart attack), moyo kushindwa kufanya kazi (Heart Failure), kufanya moyo kuwa mkubwa, ugonjwa wa figo na kupunguza nguvu za kiume.
Lakini taarifa hiyo, ilisema ili kuepuka kupata ugonjwa wa shinikizo la juu la moyo kwa kufanya mazoezi, kuzingatia lishe bora kwa kula matunda, mboga mboga, vyakula vyenye madini ya potassium vile vile kupunguza kula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha mafuta na chumvi.