NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
WAJAWAZITO wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU) wanaotumia dawa za kufubaza makali ya virusi hivyo (ARVs), hupunguza hatari ya kuwaambukiza watoto walio tumboni kwa kiwango cha chini ya asilimia tano.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam juzi na Kaimu Balozi wa Marekani hapa nchini, Immi Patterson, wakati wa uzinduzi wa filamu ya pili inayoelimisha jamii juu ya ugonjwa huo.
Alisema Serikali ya Marekani kupitia Mfuko wa Rais wa Kudhibiti Ukimwi (PEPFAR), imetumia zaidi ya dola trilioni 4.5 katika kupambana na Ukimwi nchini.
“Kupitia mfuko huo, leo hii watu bilioni moja duniani wanatibiwa, wakiwa na mama wanaotumia dawa za ARV’s ambao wanapunguza hatari ya kuambukiza watoto wao tumboni kwa kiwango cha chini ya asilimia tano.
“Tumetoka mbali katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, kilikuwa kisicho na matumaini, mtu alipopimwa na kugundulika kuwa na maambukizi ya VVU ilikuwa ni sawa na adhabu ya kifo, lakini sasa tuna fursa ya kuudhibiti ugonjwa huu ipasavyo, hata hivyo inahitaji uwajibikaji wa pamoja,” alisema.
Alisema filamu hiyo iliyozinduliwa itasaidia kupeleka ujumbe sahihi kwa jamii kuhusu ugonjwa huo na hivyo kila mmoja kuchukua hatua ikiwamo kupima kujua iwapo ana maambukizi au laa.
“Waigizaji hawa hawajawahi kuigiza mahala popote kabla, ni mara yao ya kwanza na walichukuliwa moja kwa moja katika jamii, ni watu halisi, ilioneshwa kwa mara ya kwanza jijini London na katika matamasha kadhaa likiwamo la Pan Africa huko Los Angeles mwaka huu,” alisema.
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi alisema inatia uchungu kuona bado kuna watu hawajitokezi kupima na wanapoteza maisha kwa ugonjwa huo wakati huduma za uchunguzi na tiba zinatolewa bila malipo nchini.
“Kuna kiwango kidogo cha watu katika jamii ambao wana maambukizi, changamoto ni kwamba hawajitokezi kupima kujua hali zao, hivyo naamini filamu hii itasaidia kuwafikishia ujumbe kundi hili,” alisema.