Mkoa wa Arusha umejipanga kulinda mji kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya CCTV- kamera.
Mfumo huo utawezesha mji kulindwa kwa saa 24 dhidi ya uhalifu kwa raia, mali, wawekezaji na watalii.
Kauli hiyo ilitolewa leo mjini Arusha na Mkuu wa Mkoa huo Mrisho Gambo ofisini kwake mara baada ya kutembelewa na Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnite aliyekuwa ameambatana na ujumbe wake wa Wabunge kutoka nchini Sweden.
RC Gambo alisema, mkoa huo tayari umekwisha kuonyesha nia ya kuwekeza katika mfumo huo ili kuwaongezea wananchi na mali zao usalama zaidi kwani Arusha ndio kitovu cha utalii hapa nchini.
Balozi Rangnite alisema kuwa Sweden inayo wataalamu waliobobea katika mifumo ya usalama na kumtaka Gambo kuwasilisha kwake maandiko ya vitu vinavyohitajika ili kuwezesha kutekelezwa kwa mradi huo.