LONDON, ENGLAND
KLABU ya Arsenal imethibitisha kuachana na mshambuliaji wake, Muingereza, Danny Welbeck pamoja na nyota wengine saba wakiwamo kipa, Petr Cech pamoja na beki wa kulia, Stephan Lichtsteiner.
Welbeck mwenye umri wa miaka 28, aliyejiunga na Arsenal mwaka 2014, akitokea Manchster United, ambapo alifanikiwa kutwaa mara mbili ubingwa wa Kombe la FA chini ya Arsene Wenger.
Hata hivyo amekuwa akiandwama na majereha ya mara kwa mara, sababu inayotajwa kuchangia kutupiwa virago.
Upande wa Petr Cech, yeye mwenyewe aliweka wazi kuwa anastaafu kucheza soka, huku akihusishwa kujiunga na timu yake ya zamani Chelsea kuchukua nafasi ya ukurugenzi wa ufundi.
Lichtsteiner aliyeichezea Arsenal michezo 23 katika mashindano yote msimu uliyopita, ameonekana kutoridhishwa na nafasi anayopata ya kucheza na kuamua kutumia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram kuelezea kusikitishwa na jambo hilo, tayari klabu imempa uhuru wa kuondoka.
Lakini pia Arsenal wamepanga kuwapa mkono wa kwa kheri, beki wa kushoto, Cohen Bramall mwenye umri wa miaka 23, Charlie Gilmour, pamoja na beki wa kati, Julio Pleguezuelo.
Mbali na nyota hao, awali wakati ligi inaendelea, Aaron Ramsey alikuwa mchezaji wa kwanza kuonyesha nia ya kuondoka, ambapo alisaini mkataba wa awali wa kuijunga na Juventus atakayoichezea msimu ujao.
Taarifa fupi iliyotolewa na tovuti ya klabu hiyo inaeleza kwamba:“ Tunawashukuru wote kwa mchango wenu mahali hapa, tunaomba tuwatakie kila la kheri mtakapofanikiwa kuhudumu.”
Licha ya taarifa hiyo kutowataja majina nyota hao, lakini inaelezwa hawapo katika mahitaji ya kocha, Unai Emery kwa msimu ujao, kwani hivi sasa yupo katika mawindo ya kuwanasa nyota wangine wapya.