NA BADI MCHOMOLO
ANTHONY Davis, hakuwa na jina kubwa sana katika kipindi cha misimu ya hivi karibuni kutokana na uwezo wake wa kikapu kufanana na wachezaji wengine ambao majina yao husikika kwa muda.
Nyota huyo wa kikapu amekuwa na mchango mzuri ndani ya kikosi chake cha timu ya New Orleans Pelicans ambayo inashiriki ligi kuu ya mchezo huo nchini Marekani.
Ana umri wa miaka 23, lakini kwenye kikosi hicho amekuwa akisambaza mipira kutoka nyuma hadi langoni kwa wapinzani wake na wakati mwingine anaweza kusimama mbele na kufunga mwenyewe.
Kutokana na uwezo huo ambao ameuonesha msimu huu kwenye michuano ya NBA, aliweza kujipatia nafasi ya kuchaguliwa kwenye kikosi cha NBA All Star Game kwa upande wa timu ya Western Conference ambapo fainali ilipigwa Februari 19 dhidi ya Eastern Conference na Western wakatwaa ubingwa.
Western ni timu ya nyota wa kikapu ambao wanatoka ukanda wa Magharibi nchini Marekani kukiwa na umoja wa timu 15 ambazo zinatafuta wachezaji ambao wanaweza kuwakilisha ukanda huo dhidi ya wapinzani wao wa Eastern Conference, ambapo pia kuna timu 15.
Katika kikosi cha Western Conference, kinaundwa na mastaa ambao wanafanya vizuri kwa sasa kwenye Ligi ya NBA kama vile Stephen Curry kutoka Golden State Warriors, Kelvin Durant, Klay Thompson, James Harden wa Houston Rockets na wengine wengi.
Wakati huo kwa upande wa Eastern Conference, nyota wanaounda kundi hilo ni pamoja na LeBron Jame wa Cleveland Cavaliers, Carmelo Anthony wa New York Knicks na wengine wengi.
Kati ya wachezaji hao wa pande zote mbili, nyota wawili, LeBron James wa Eastern Conference pamoja na Stephen Curry wa Western Conference ndio ambao walipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika fainali ya NBA All Star Games.
Lakini Anthony Davis ni nyota ambaye aliibuka na kushangaza mashabiki wengi wa kikapu kwa kuondoka na tuzo ya mchezaji bora ambayo inajulikana kwa jina la MVP.
Msimu uliopita, LeBron alichukua tuzo hiyo kutoka mikononi mwa Curry kwenye michuano ya Ligi ya NBA, hivyo wawili hao walipewa nafasi kubwa ya mmoja wao kutwaa tuzo hiyo kwenye All Star Game.
Hakuna aliyedhani kama Davis anaweza kuwatuliza wababe hao wa kikapu kwa misimu ya hivi karibuni, lakini aliweza kuweka historia mpya huku timu yake ikiibuka na ushindi wa vikapu 192-182.
Davis aliweka rekodi ya aina yake ambayo haijawekwa na mchezaji yeyote kwa kipindi cha hivi karibuni kwa kuondoka na pointi 52, wachezaji wengi wanaishia pointi 40 lakini yeye aliwashangaza watu kwa aina yake.
“Sikudhani kama ningeweza kuweka historia yangu mbele ya wababe wa mchezo huo kama vile Curry na LeBron, ambao wana uwezo mkubwa kwa sasa.
“Mwalimu wangu aliniambia kwamba, kila nikipata mpira niwe na lengo la kupachika kikapu na ndivyo nilivyofanya hadi kuweza kuisaidia timu kutwaa ubingwa pamoja na kujichukulia tuzo ya MVP, hii ni historia kubwa sana kwangu.
“Wakati tupo katika chumba cha kubadilishia nguo baadhi ya wachezaji wenzangu waliniambia kuwa kila muda watakuwa wananipa mpira hivyo kazi yangu ni kufunga tu, James Harden na wengine waliniambia na ndio maana naweza kusema wamenifanya niwe hapa,” alisema Davis.
Pointi hizo 52 ambazo alizipata Davis zilitokana na jumla ya mitupo 39 ambayo aliitupa na kumfanya awe mfalme wa fainali hiyo.
Nyota wa zamani wa kikapu ambaye aliwahi kuweka rekodi ya pointi nyingi ni Wilt Chamberlain, wakati anakipiga katika timu ya Philadelphia mwaka 1962, ambapo alipata pointi 42.
Lakini katika kipindi cha hivi karibuni nyota mbalimbali kama vile Curry, LeBron na Kobe Bryant waliweza kufikisha pointi zaidi ya 39.
Kwa sasa Davis ameweka jina kubwa kwenye mchezo huo ikiwa ni msimu wa 2014-15 katika kuwania tuzo ya MVP alishika nafasi ya tano, wakati huo Curry akiibeba tuzo hiyo.