Na FREDERICK FUSSI
UCHAGUZI wa Shirikisho la Soka barani Afrika CAF uliofanyika Machi 16, 2017 katika Jiji la Addis Ababa nchini Ethiopia na kumng’oa madarakani aliyekuwa Rais wa shirikisho hilo aliyeingia madarakani akiwa na umri wa miaka 42 na kuondoka kwa aibu akiwa na miaka 71 na kudumu madarakani kwa jumla ya miaka 29 tangu Machi 10, 1988, Issa Hayatou raia wa Cameroon umeonesha kuwa siasa za Afrika zinafanana na kwa hakika siasa za soka hazina tofauti na siasa za uchu wa madaraka kwa viongozi wa kiserikali barani Afrika.
Issa Hayatou anatajwa kama mwanaume wa shoka katika uwezo wake wa kuendelea kung’ang’ania madaraka ya kuongoza gurudumu la maendeleo ya soka barani Afrika. Kitendo cha Hayatou kukaa madarakani kwa muda mrefu si jambo geni katika siasa za Bara la Afrika. Moja kati ya mambo ambayo yamelirudisha Bara la Afrika nyuma ni pamoja na kuwa na fikra zile zile katika nyanja za madaraka jambo linalozuia kabisa fikra mpya na zilichochangamka zaidi kuingia madarakani na kuleta mabadiliko.
Kung’oka kwa Hayatou kunaendelea kutoa fundisho kwa viongozi zaidi ya 10 wa Afrika katika ngazi ya wakuu wa nchi na Serikali wanaoendelea kufurahia kikombe cha madaraka bila kujali kuwa nchi za Afrika si mali yao binafsi bali ni tunu na zawadi kwa kila Mwafika.
Uchaguzi wa CAF umemuingiza madarakani Rais Mpya wa shirikisho hilo la Soka, Ahmad Ahmad aliyekuwa Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini Madagascar alipigiwa kura na wakuu wengine wa mashirikisho ya soks kutoka mataifa 52 barani Afrika. Inawezekana Afrika ikiwa nyuma kimaendeleo iwe ni kweye soka au kwenye siasa za kawaida kutokana na si tu kwa sababu ya watu wanaong’ang’ania madaraka lakini pia watu wenye mamlaka na uwezo wa kuwatoa madarakani wang’ang’anizi wa madaraka.
Pamoja na kuwa Hayatou alidumu madarakani kwa jumla ya miaka 29 lakini bado akawa na matamanio ya kutaka kuendelea kuwa Rais wa Shirikisho hilo la soks la Afrika. Unaweza kujiuliza swali moja, amedumu madarakani kwa miaka 29, Je, kuna jambo gani jipya ataweza kulifanya endapo angechaguliwa upya kuendelea kushika wadhifa huo? Kadhalika viongozi wengine wa bara la Afrika wanaoendelea kung’ang’ania madarakani wana mambo yApi mapya ya kuendelea kuyafanya?
Wakati hayo yanAendelea kwenye soka niliwahi kuandika hapa awali kuhusu yaliyojirika katika Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.
Viongozi wa Umoja wa Afrika walikutana kati ya Januari 22 na 31 , 2017 huko nchini Ethiopia katika Mji Mkuu wa Adis Ababa. Mkutano huu wa Umoja wa Afrika uliokutanisha wakuu wa nchi na Serikali ulifanyika wakati ambapo umajuhui wa Afrika unakwamishwa na ubovu wa demokrasia katika bara lote jambo ambalo limetishia mafanikio ya nchi hizi za dunia ya tatu kama ambavyo zimebatizwa jina hilo na nchi zilizoendelea sana kiviwanda duniani.
Wiki nne kabla ya Mkutano huo kufanyika ambapo tulishuhudia kuendelea kuporomoka kwa misingi ya kidemokrasia katika mataifa mengi ya Afrika; ukiwamo ule mgogoro wa aliyekuwa Rais wa Gambia, Yahya Jammeh kugoma kuachia madaraka mpaka alipotishiwa kuondolewa kijeshi na Umoja wa Kiuchumi wa Jumuiya ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS). Jammeh anatuhumiwa kuondoka Gambia na mabilioni ya dola ambazo ni fedha za umma!
Mkutano huo wa 28 wa Umoja wa Afrika ulikuwa unafanyika wakati nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo nayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Afrika; Rais wake Joseph Kabila muda wake wa kuwapo madarakani uliisha tangu Disemba 2016 lakini Rais huyu amebakia madarakani mpaka hivi sasa jambo lililozua tafrani na taharuki nchini humo kutokana na kitendo hicho kwenda kinyume na Katiba ya nchi hiyo na kutoonekana kwa dhamira ya wazi na ya dhati kwa kiongozi huyo kuachia madaraka.
Wakati hayo yanaendelea huko nchini Congo DRC, bado Afrika ina jumla ya marais 10 ambao wamedumu muda mrefu madarakani kwa njia ya ukandamizaji wa demokrasia na utawala wa mabavu na ubabe mwingi dhidi ya wapinzani wao kisiasa ambao kimsingi ni Waafrika wenzao. Nchi ambazo zimekuwa na watawala waliokaa muda mrefu madarakani na kukandamiza demokrasia katika Mataifa yao ni pamoja na Rais Paul Kagame wa Rwanda miaka (23) madarakani tangu mwaka 1994, Rais Isaias Afwerki wa Eritrea aliyedumu madarakani miaka (24) tangu mwaka 1993, Rais Omar al-Bashir wa Sudan aliyedumu madarakani kwa jumla ya miaka (28) tangu mwaka 1989.
Wengine ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliyedumu madarakani kwa miaka tangu mwaka 1986 aliyeingia madarakani baada ya kumpindua Rais Milton Obote, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ambaye hivi sasa ana miaka 93 na amedumu madarakani kwa miaka (37) tangu mwaka 1980, Rais Paul Biya wa Cameroon nchi ambayo Hayatou ametokea, huyu Biya amedumu madarakani kwa miaka (35) tangu mwaka 1982, Rais José Eduardo dos Santos wa Angola aliyedumu madarakani kwa miaka (38) tangu mwaka 1979, Rais Teodoro Obiang Nguema Mbasogo wa Equatorial Guinea huyu amedumu madarakani kwa muda wa miaka (35) tangu mwaka 1979, Rais Idriss Déby wa Chad ambaye amedumu madarakani kwa miaka (27) tangu mwaka 1990 na wa mwisho ni Rais Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Congo aliyedumu madarakani mara mbili mara ya kwanza aliingia madarakani February 8, 1979 na kuondoka Machi 15, 1992 (miaka 13) akaona haridhiki akarejea tena madarakani Oktoba 25, 1997 na yupo madarakani mpaka leo hii. Hawa ndio watawala na si viongozi wa Bara la Afrika,
Umoja wa Afrika wenyewe kuwa tu na lundo la viongozi wenye uchu wa madaraka, waliokaa madarakani bila kuzingatia demokrasia ya kupokezana vijiti vya uongozi unajigeuza kuwa genge la watawala wabovu wanaotumia nguvu kukandamiza uhuru wa Waafrika wenzao katika mataifa yao.
Hakuna asiyejua shubiri na maisha magumu wanayoyapata wapinzani wa kisiasa wa watawala wenye mabavu Katika nchi mbalimbali za Afrika.
Wakati hayo yanaendelea katika mataifa mengine Afrika hapa nchini tayari tumeona viongozi kadhaa wa upinzani wakibambikiwa kesi za kisiasa na kutupwa gerezani kwa vifungo au kunyimwa dhamana. Ninyi ni mashahidi wa yote yanayoendelea hivi sasa nchini Tanzania kuhusu changamoto za mwingiliano wa kimadaraka kati ya mihimili ya dola.
Siku kadhaa zilizopita mmeshuhudia namna ambavyo mtunga sheria na mbunge aliyeaminiwa na wananchi na wapiga kura wake alivyosoteswa rumande kwa muda wa miezi minne na hatimaye Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu kutamka kuwa mbunge huyo aliwekwa rumande kwa kunyimwa dhamana kinyume na utaratibu wa kisheria na haki katika mfumo wa kutoa haki. Hii ndio Afrika yetu.
Maendeleo ya Bara la Afrika changamoto yake kubwa ni kupambana wenyewe kwa wenyewe. Kuendelea kwa Bara la Afrika kunategemea kiwango cha umoja wa kitaifa uliopo ndani ya kila Taifa. Lakini madaraka yamekuwa na nguvu kubwa kuzidi umoja wetu wa kitaifa katika mataifa yetu.
Maendeleo ya Bara la Afrika ni ya kasi ndogo sana kwa sababu ya kutoisha kwa migogoro ya kisiasa ambayo chanzo chake ni uchu wa madaraka. Nchini Afrika Kusini Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma alinusurika kung’olewa madarakani kwa kashfa ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa kutumia fedha za umma kufanya ukarabati wa nyumba yake binafsi. Hawa ndio viongozi wa Kiafrika tunaowategemea waliondoe bara letu kwenye lindi kubwa la umasikini.
Tukifaulu kuwafanya viongozi wetu na sisi wenyewe kuheshimu misingi ya kidemokrasia kama ilivyo, bila shaka tutaweza kuliunganisha Bara la Afrika kuwa moja na kutimiza ndoto ya umajuhui wa Afrika na kuwa na Taifa moja kubwa la Afrika lenye nguvu duniani kama ilivyo kwa Marekani.
Bado hatujachelewa kurekebisha kasoro zetu za kidemokrasia japokuwa tuna safari ndefu ya kuwa na demokrasia ya kweli Afrika.