KUNA baadhi ya watu wapo kwenye mahusiano ambayo wanajua fika hayana faida kwao, lakini wapo tu. Kila kukicha ni kulalamika, lakini haondoki, yupo tu, mwenyewe anadai anavumilia.
Yupo msomaji mmoja alinisimulia kisa kilichonisisimua sana. Alikuwa na mpenzi wake ambaye walipendana sana, hadi kufikia hatua ya kutambulishana kwa wazazi na kupanga mipango mingi ya kimaendeleo juu ya maisha yao na familia wanayoitarajia.
Lakini cha kustaajabisha, mwanaume hakuwa mwaminifu kwa mwanamke. Anasema kuwa alimfumania mpenzi wake mara mbili lakini bado aliendelea kuwa naye akitarajia atabadilika, kilichotokea ilikuwa kinyume na matarajio yake na kumpelekea jeraha la moyo.
SIKIA SIMULIZI YAKE
“Niliumia sana baada ya kumfumania mpenzi wangu na mwanamke mwingine, lakini nilimsamehe baada ya kukiri kosa lake na kuahidi kutorudia tena kwani ni shetani alimpitia. Lakini haikupita mwezi nikamfumania tena na mwanamke mwingine tofauti na yule wa kwanza.
“Niliumia sana, tena safari hii hakuniomba msamaha badala yake mimi ndiye nilimuomba msamaha. Nilijiona kama kama siwezi kupata mwenzi mwingine. Nikafikiri muda ambao tulikaa, nikahisi sitaweza kwenda kuanzisha uhusiano mpya, kwa kifupi nilimzoea sana.
“Baada ya mwaka, nikashindwa kuvumilia na kuanzisha uhusiano na mtu mwingine, tulidumu kwa mwaka mmoja tu baada ya mpenzi wangu wa mwanzo kuniangukia na kuniomba msamaha. Alisema anajutia makosa yake nami ndiye mwanamke sahihi wa maisha yake. Aliniomba nirudi kuwa naye na kuahidi kunipenda kwa dhati na kupanga upya.
“Kuonyesha nia yake tulifungua biashara ya pamoja. Inasikitisha sana kwani ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tu niligundua ana msururu wa wanawake aliojihusisha nao kimapenzi.
“Ilinibidi nifanye maamuzi ya kuachana naye ingawa niliumia na bado nilimpenda na kupata jeraha la moyo kwa mara ya nyingine,” anasimulia msomaji huyo.
Unaweza kuona ni kwa namna gani alipitia kipindi cha mateso katika maisha yake. Lakini je, ni sahihi kuendelea kumng’ang’ania hata kama anakutesa?
Inawezekana nawe unalo tatizo kama hilo. Je, maumivu yanavumilika? Katika vipengele vifuatavyo hapa chini vitakupa mwanga wa nini cha kufanya.
TAMBUA THAMANI YAKO
Ukishajua thamani yako, hutakuwa wa kuumizwa kila siku katika mapenzi. Tambua kuwa una thamani kubwa hata kama mwenzi wako haioni.
Amini kwamba unaweza kupata mtu mwenye kukuelewa, kukupenda kwa dhati na kuheshimu hisia zako. Hakuna mtu aliyeumbiwa matatizo bali sisi wenyewe ndiyo husababisha hayo matatizo.
Kama haioni thamani yako kwa nini umng’an’ganie? Mtu mwenye mapenzi na wewe lazima ataona thamani yako na kukuthamini. Umeachana naye na imepita miezi zaidi ya sita au mwaka, baada ya kipindi hicho kirefu anataka mrudiane, hushtuki?
Jiulize kwanza kwa nini? Alichokimbia mara ya kwanza ni nini na kinachomrudisha ni kipi? Amehangaika huko ndiyo anarudi kwako baada ya kushindwa huko alikotoka.
Ina maana kwamba muda huo ndiyo anakuona umeongezeka thamani? Ukishajua thamani yako, mtu hawezi akaondoka kwa kiburi na kurudi anavyotaka kama nyumba ya kupanga!
JIAMINI
Tunapaswa kujiamini kwa kila kitu tunachofanya katika maisha. Udhaifu ni kati ya sifa za binadamu lakini kujiamini ni njia pekee inayomfanya mtu afanikishe lile analolihitaji.
Jiamini kwamba hata bila yeye unaweza kuishi, jiamini. Kwanini hujiamini? Eti nikiachana na huyu siwezi pata mwingine kama yeye! Hapana si kweli. Pengine yupo mwingine, sahihi zaidi, ambaye alikuwa anakusubiri kwa muda mrefu.
AMUA KWA AJILI YAKO MOYO WAKO
Ni vyema kufanya maamuzi magumu ila yaliyo sahihi kuliko kuumia. Kwani ukiwa huna furaha katika uhusiano, hata vitu vingine pia vya kimaendeleo hutavifanya kwa uyakinifu. Kuachana na mtu ambaye bado unampenda ni jambo gumu sana, lakini pia kukuonyesha usaliti uliowazi ni suala jingine ambalo halivumiliki. Kuna tabia ambazo zinavumilika katika mahusiano, lakini usaliti hapana.
Kumfumania mtu zaidi ya mara mbili na kuendelea naye ni uoga wa kufanya maamuzi. Ni vyema kufanya maamuzi ambayo una hakika hutageuka nyuma na kusonga mbele.
Kufanya maamuzi ya kuvunja uhusiano leo na baada ya kipindi kurudiana na huyo mtu siku zote huwa na hasara kuliko faida. Angalia moyo wako, fikria kuhusu maisha yako.
Una sababu gani ya kuuacha moyo wako kwa asiyejua thamani yako? Amua sasa.
Jiandae kusoma kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitaingia mitaani hivi karibuni.