Zainab Iddy -Dar es salaam
KAMA ulikuwa unadhani kiungo fundi wa kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Simba,Jonas Mkude amelala tu kipindi hiki cha janga la corona utakuwa unajidanganya.
Ipo hivi kutokana na janga la corona linaloendelea kuumiza vichwa vya wataalamu wa afya ulimwenguni kote, Jonas Mkude ameamua kuweka mambo yote pembeni na kutumia muda mwingi katika fukwe za Cocobeach jijini Dar es Salaam kujifua.
Jana kupitia mitandao mbalimbali ya kijamiii, ilionekana video iliyokuwa ikimuonyesha Mkude akiwa katika mazoezi mazito ya kusaka pumzi.
Katika video hiyo, Mkude alionekana akiwa amefunga kamba tairi la gari kubwa kisha kujifunga kiunoni na kukimbia nalo kwenye eneo la mchanga.
Hiyo ni picha ya kwanza ya Mkude kuonekana hadhari akiwa katika mazoezi tangu Simba ilipovunja kambi yake kutii agizo la serikali ambayo imepiga marufuku shughuli zinazosababisha mikusanyiko ya watu ikiwemo michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuepuka kusambaa virusi vya corona.
Mkude aliliambia MTANZANIA jana kuwa, kutoonekana kwa picha zake za mazoezi kama ilivyo kwa nyota wengine, haina maana amekaa tu bali hapendi mambo yake yawe hadharani.
“Sipendi kila mtu ajue nafanya kitu gani katika maisha yangu na hata suala la mazoezi nafanya kila siku asubuhi na jioni kwenye mazingira tofauti kwani najua jukumu langu ni kuwa fiti muda wote.
“Video iliyoonekana nilikuwa katika harakati za kufanya mazoezi ya kutafuta pumzi, kuongeza nguvu ya miguu pamoja na kuifanya akili ifanye kazi kwa haraka muda wote, baada ya ligi kurejea watakaokuwa wananizuia kufanya kazi yangu uwanjani wajiandae,”alisema Mkude.
Mkude ni miongoni mwa viungo bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo amekuwa mhimili mkubwa katika kikosi cha Simba kwa miaka mingi sasa.