Mohamed Hamad -Kiteto
MKAZI mmoja wa Mtaa wa Logoto wilayani Kiteto mkoani Manyara, Shedrack Sekeyani (40), amemuua mke wake kwa kumnyonga kisha naye kujinyonga.
Shedrack alimuua mke wake, aliyefahamika kwa jina la Magdalena Sirai (30), usiku wa kuamkia Aprili 1, 2020 sebuleni kwake huku watoto wake akiwepo Rejina Shedrack (12), Faraja shedrack (7), Babu Shedrack (5) na Ziki Shedrack (3) ambao walishuhudia tukio hilo.
Tukio hilo limevuta hisia za watu wengi baada ya kusikia vifo hivyo vya wanadoa hao kutokana na wivu wa mapenzi.
“Baba aligombana na mama usiku, akaanza kumpiga…nilimwomba amsamehe, aliendelea kunyonga mpaka mama aliponyamaza, kisha yeye akatutaka tufunge mlango na kutoka nje, tukaendelea kuwa ndani, kwa sababu baba ni mkali, tulihisi angetudhuru na sisi,” alisema mtoto mkubwa Regina Shedrack.
Alisema ilipofika asubuhi ya saa 12, alitoka nje na kumkuta baba yao huyo akiwa ananing’inia juu ya mti wao aina ya Mgunga uliopo nje ya nyumba yao jambo lililowafanya kukimbia kwenda kwa mjomba wake kumweleza hali hiyo ambapo ndugu wa marehemu walifika katika eneo la tukio na kushudia miili hiyo.
“Baada ya kuwaeleza wajomba zetu na kisha majirani ambao wengi wao tuliwaarifu kwa kupiga mayowe ambapo walifika kwa haraka na kushuhudia hali hiyo,” alisema mtoto huyo
Kwa upande wake Mjumbe wa Shina, Jastine Emmanuel alisema alipigiwa simu ambapo alimjulisha Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Logoto, Mwinjuma Suphiani, ambaye alifika katika eneo hilo na kisha kupiga simu polisi ambao walifika katika eneo la tukio.
“Nilipigiwa simu na Samson Tumaa, mjomba wa watoto wa marehemu hao nikiwa kazini kwangu, mapema kabisa asubuhi juu ya tukio hilo nikazimika kujulisha uongozi wa ngazi ya juu yangu ambao walifika kwa wakati na hatua kuanza kuchukuliwa,” alisema
Diwani wa Kata ya Bwagamoyo, Yahaya Masumbuko (CCM), akizungumzia tukio hilo alisema mbali na vifo hivyo, hivi karibuni miezi miwili iliyopita, mwanamke mmoja katika eneo lake pia alikatisha maisha kwa kujinyonga
Alisema vitendo hivyo vinachangia ongezeko la watoto yatima ambao mara nyingi wanakosa huduma muhimu toka kwa wazazi wao na kutegemea watu wengine ambao nao hawawezi kuzitoa kama ilivyo kwa wazazi wao
Samson Tumaa mjomba wa watoto hao, alisema kuwa kwa sasa aendelea kuwalea watoto hao mpaka vinginevyo itakavyoamriwa na familia pamoja na viongozi wao wa mila kwa kuwa wengine wanasoma ili waweze kupata haki yao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George Kasabago amethibitisha vifo hivyo na kuwataka wananchi kutojichukulia sheria mikononi kwani kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.