26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Amina: Nilipata mimba nikiwa Mwanafunzi

Na Patricia Kimelemeta, Mtanzania Digital

WAKATI Serikali inatekeleza Programu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) ambayo inalenga watoto kuanzia umri sifuri hadi miaka minane, kuna baadhi ya watoto wamezaliwa kutokana na changamoto mbalimbali walizopata mama zao ikiwa ni pamoja na kubakwa au kuolewa wakiwa na umri mdogo.

Amina Omary (19) mkazi wa Temeke-Dar es Salaam alipata mimba akiwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza baada ya kubakwa na kujifungua mtoto wa kiume.

“Nilikatisha ndoto zangu za kuwa muuguzi baada ya kubakwa na kupata ujauzito nikiwa kidato cha kwanza, wakati huo nilikuwa naishi kwa mjomba wangu Mtwara vijijini, nililalizima kuacha shule na kukaa nyumbani ili nisubili kujifungua na baada ya kujifungua sikubahatika tena kurudi shuleni.

“Kutokana hali ngumu ya maisha kwenye familia yangu, baba alifariki na mama alikuwa akiishi mwenyewe kwa kutegemea kilimo, kwa hiyo suala la kubakwa likamalizwa kwenye ngazi ya familia na mpaka sasa mtoto wangu yupo ana umri wa miaka.mitatu mwenye afya kamili anaishi na mama yangu kijijini,” amesema Amina.

Ameongeza kuwa, Kwa sasa anafanya kazi ya kuuza duka na mshahara anaoupata anamtumia mama yake Kwa ajili ya Malezi ya mtoto.

“Ni kweli maisha yangu sio mazuri kivile, lakini sikukata tamaa, nilikua Dar es Salaam kutafuta kazi nikapata ya kuuza duka la nguo na mshahara wangu ninaoupata namtumia mama kwa ajili ya kulea mtoto wangu na watoto wengine wa ndugu zangu,” amesema.

Hata hivyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima akizungumza hivi karibuni wakati akitoa taarifa ya matukio ya ukatili kwa watoto katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 amesema, jumla ya matukio yaliyoripotiwa ndani ya Jeshi la Polisi ni 11,499 ikilinganishwa na matukio 15,870 katika kipindi kama hicho mwaka 2020, sawa na upungufu wa imatukio 4,371 ikiwa na asilimia 27.5

Amesema kuwa, Mkoa wa Kipolisi Ilala uliopo Dar es Salaam ni miongono mwa maeneo yanayoongoza kwa vitendo hivyo.

“Mikoa iliyoongoza ilikuwa ni Arusha (808), Tanga (691), Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489).

Amesema kuwa makosa yanayoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na ulawiti (1,114).

Amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara yenye dhamana na watoto iliandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 ambayo imeainisha Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ikiwepo Haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa.

Amesema kuwa, sambamba na kuratibu utungwaji wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Taasis isiyo ya Kiserikali ya Kaya Foundation, Piliana Ngome amesema kuwa, kuna baadhi ya watoto wamezaliwa wakati wazazi wao wamepitia madhira mbalimbali ikiwamo kubakwa, kupata mimba wakiwa na umri mdogo au kuachishwa shule na kulazimishwa kuolewa bila ridhaa yao.

Amesema kuwa, watoto hao (wazazi na watoto waliozaliwa) wanahitaji kupewa elimu ya saikolojia ili waweze kujitambua na kuamini kuwa bado kuna maisha mengine yanendelea na sio kukata tamaa.

“Tunapaswa kuwapa elimu ya kujiamini, kujitambua na kusonga mbele na sio kukata tamaa kwa sababu alibakwa au alizaliwa katika mfumo wa ukatili, wanapaswa kujua kuwa maisha bado yanendelea, wanapaswa kusoma Kwa bidii na kusonga mbele ili waweze kutimiza ndoto zao hata kama walikwama njiani, wanaweza kutafuta njia mbadala ya kujikwamua,” amesema Ngome.

Ameongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho kuna taasisi mbalimbali zinajitolea kwa ajili ya kuwasaidia vijana waliopata madhira hayo, wanapaswa kujitokeza kwenye taasisi hizo na kutoa taarifa zao ili waweze kusaidiwa kwa namna moja au nyingine.

“Kufanyiwa ukatili sio mwisho wa maisha, sio njia ya kukata tamaa, bali tunapaswa kusimama na kusonga mbele, wajitokeze kwenye ofisi za serikali kutoa taarifa zao au taasisi zinazowasaidia ili waweze kupata usaidizi wa aina yoyote ile,” amesema.

Hata hivyo, Ofisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Nyamara Elisha amesema kuwa, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuwalinda na kuwatetea watoto katika msingi wa malezi jumuishi.

Amesema kuwa, kila mtu ana wajibu wa kuhakikisha anamlinda mtoto kwa namna yoyote ile na pale anapoona kuna viashiria vya vitendo vya ukatili wanapaswa kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe kabla ya kutoka tukio.

“Malezi yenye mwitikio yanamtaka Kila mwana jamii kushiriki kulea na kumlinda watoto, ndio maana tunaendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kutambua umuhimu wao katika malezi,” amesema Elisha.

Ameongeza kuwa, mpaka sasa Serikali imeweza kugatua madaraka kuanzia ngazi ya kata ambapo Kuna maofisa Ustawi wa Jamii, maofisa Maendeleo ya jamii na ngazi ya mtaa kuna viongozi ambao wanapewa mafunzo ya namna ya kuwalinda watoto na kutoa taarifa pale inapotokea tukio la aina yoyote ambalo lisilo la kawaida.

Hata hivyo, PJT-MMMAM inatekeleza afua tano za lishe,afya, elimu, malezi yenye mwitikio, ulinzi na usalama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles