23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYEPIGA PICHA NYUFA MAJENGO UDSM AELEZA ALIVYONUSURIKA KUTEKWA

 

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kumbusho Dawson, aliyepiga picha za hosteli mpya za chuo hicho zilizoonyesha majengo hayo kuwa na nyufa, amedai Januari 11 mwaka huu alinusurika kutekwa watu ambao bado hajawatambua akiwa eneo la Mlimani City,   Dar es Salaam.

Desemba 4 mwaka jana, Dawson alikamatwa na   polisi na kuwekwa ndani katika Kituo cha Polisi Oystebay akituhimiwa kusambaza picha zilizoonyesha nyufa za hosteli hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dawson aliyesema amekwisha kuripoti tukio hilo polisi.

Alisema tangu mwaka jana baada ya kupiga picha hizo na kuzisambaza, amekuwa akifuatiliwa na watu wawili kila mahali anapoenda.

Mwnafunzi huyo alisema hawezi kulihusisha tukio hilo la kufuatiliwa moja kwa moja na picha alizosambaza, lakini kinachomshangaza ni watu hao kuanza kumfuatilia baada ya kusambaza picha hizo.

“Tangu mwaka jana baada ya mimi kupiga picha katika mojawapo ya hosteli mpya zilizojengwa na TBA (Wakala wa Majengo Tanzania) iliyokuwa ikionyesha nyufa kumekuwa na watu ambao wamekuwa wakinifuatilia mara kwa mara kila mahali ninapoenda.

“Siwezi kusema kupiga picha za nyufa ndiyo sababu ya kunifuatilia kwangu au la.

“Awali nilidhani labda wana shughuli zao lakini kilichonishangaza ni kadiri siku zinavyozidi kwenda nikikaa sehemu watu hawa nao walikuwa wanakaa umbali kidogo nilipo mimi.

“Nikianza kuondoka, nikigeuka nyuma nawaona wananifuatilia ndipo nilipogundua kuwa nia yao haikuwa nzuri,”alisema.

Alivyonusurika kutekwa

Dawson ambaye pia ni kiongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), alisema Januari 11 mwaka huu, akitoka Mlimani City alianza kutembea kwa miguu kurudi hosteli lakini mbele yake akaona gari ya Toyota Noah ikiwa imeegesha mlango ukiwa wazi.

“Nilivyofika kwenye lile gari wale watu walinitaka niingie kwenye gari. Niliwajibu mnanifahamu na mnajua ninakoenda?

“Wakati nikiwauliza maswali haya, walianza kushuka kwenye gari huku wakiniambia si lazima niwajue wao ni kina nani, wakaniambia kwa ukali niingie kwenye gari haraka,’alisema.

Alisema anamshukuru Mungu kwa sababu wakati wa purukushani zilizochukua takribani dakika moja na watu hao, alianguka huku akipiga kelele ndipo watu waliokuwa jirani wakiwamo madereva bajaji wakamsaidia.

“Baada ya purukushani zile nilipiga kelele kuwa wanataka kuniteka, baada ya kupiga kelele wale watu  waliokuwa wananilazimisha nipande katika gari lao waliingia haraka kwenye gari na kuondoka.

“Kwa pekee niwashukuru waendesha bajaji kwa msaada wao, hakika bila wao leo tungekuwa tunazungumza mambo mengine,”alisema Dawson.

Jitihada za kuupata uongozi wa Mlimani City kuzungumzia tukio hilo hazikuzaa matunda  jana baada ya kufika ofisini hapo na kuambiwa kuwa mwenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo   alikuwa amekwisha kuondoka kazini.

Hata hivyo, mfanyakazi mmoja wa Mlimani City ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema:

“Lakini nikwambie, hatujapata taarifa za tukio la aina hiyo kwa sababu matukio yote ambayo hutokea kwenye maeneo yetu huwa tunapewa taarifa, lakini hadi sasa hatujapewa taarifa za tukio hilo,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Aripoti polisi

Alisema baada ya tukio hilo, aliripoti kwenye vyombo tofauti vya ulinzi ikiwa ni pamoja na polisi wasaidizi (Auxiliary Police) na Polisi wenyewe na kuandikiwa RB yenye kumbukumbu namba UD /RB/344/2018.

Kutokana na hilo, alisema polisi walimwomba endapo atawaona watu hao mahali popote wakimfuatilia atoe taarifa huku wakimtaka asitembee peke yake na kwamba pale atakapoona inafaa ajilinde.

“Hali kadhalika suala hili niliripoti kwa walezi wangu wanaonilea kwa maana ya Ofisi ya Mshauri wa Wanafunzi hapa chuoni kwangu,”alisema.

Aelezea alivyokamatwa na polisi

Dawson alisema siku chache baada ya kusambaza picha za nyufa za hosteli hizo alikamatwa na polisi.

Simu zake bado zinashikiliwa

Katika hatua nyingine Dawson aliliambia MTANZANIA kuwa polisi walizichukua simu zake mbili kama ana mawasiliano na baadhi ya wanasiasa.

“Siku ile walihoji kwa saa nne huku wakiwataja wabunge kama tisa hivi kuwa nina mawasiliano nao lakini katika hao walionitajia niliwaambia si kweli isipokuwa nina mawasiliano ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa kwa sababu ni mbunge wangu na mimi nimetokea Iringa na DC (Mkuu wa Wilaya) Richard Kasesela,”alisema Dawson.

Alisema tangu siku hiyo akifuatilia simu zake hizo amekuwa akiambiwa kuwa bado wanafanya uchunguzi.

“Kila nikienda wanasema wanafanyia uchunguzi na nimewaambia simu zangu zina document nyingi za shule lakini bado hawajanipatia,”alisema.

Mshauri wa wanafunzi ( dean of student) wa UDSM Pauline Mabuga, alipotafutwa ili kueleza kama kweli Dawson alifika kwake kuripoti tukio hilo, alisema yeye siyo msemaji wa chuo.

Katika hatua nyingine Dawson alisema hatua yake ya kusambaza picha hizo kwa sababu baada ya hatua yake hiyo, ukarabati umefanyika kwenye majengo hayo.

Alisema pia hatua yake ya kupiga picha hizo na kusambaza, aliifikia baada ya kuona mara kwa mara wanaripoti kwenye uongozi baadhi ya kasoro kwenye hosteli hizo lakini hakuna hatua ambazo zilikuwa zinachukuliwa.

Hata hivyo MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP, Lazaro Mambosasa, kujua kama ana taarifa za jaribio la kutekwa Dawson ambapo alisema hana taarifa yoyote kuhusu  hilo.

“Sina taarifa hizo unazoniuliza,” alijibu kwa kifupi Kamanda Mambosasa.

Alipoulizwa kuhusu kushikiliwa kwa simu za Dawson, alijibu kwa kifupi kuwa hana taarifa hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni , Jumanne Mulilo, alisema suala la kutaka kutekwa kwa Dawson hana taarifa na analisikia kutoka kwa mwandishi.

“Sisi(Polisi) kazi yetu ni kuchunguza kama kweli ametoa taarifa polisi tutachunguza na ukweli utajulikana,” alisema Mulilo.

Aliongeza kuwa madai ya Dawson ya kuwa alikamatwa na kunyang’anywa simu zake awaulize waliomkamata wameweka wapi simu zake.

“Kuhusu simu zake awaulize waliomkamata maana mimi sifahamu kama walimkamata,” alisema Kamanda Mulilo.

Habari hii imeandaliwa na Leonard Mang’oha, Tunu Nassor

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles