25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

ALIYEPANDIKIZWA FIGO MUHIMBILI AMWAGA MACHOZI YA FURAHA

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

MACHOZI ya furaha yamemtoka , wakati akiwashukuru na kuwaaga madaktari bingwa wa figo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), mbele ya waandishi wa habari jana.

Novemba 21, mwaka huu, Priscer, aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo, alifanyiwa upasuaji wa kupandikizwa figo iliyotolewa na ndugu yake, Batholomayo Mwingira.

Upasuaji huo ambao ni wa kwanza kufanyika hapa nchini, ulifanywa na madaktari wa MNH kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya BLK ya India.

Priscer alisema anamshukuru Mungu kwa uzima aliompatia hadi sasa na Serikali kwa kuiwezesha MNH kumfanyia upasuaji huo.

“Nawashukuru mno madaktari wote walioshiriki kunifanyia upasuaji huu, namshukuru pia ndugu yangu kwa kujitolea kunipa figo yake moja,” alisema.

Aliwataka wagonjwa walio katika mchakato wa kusubiri upasuaji huo na wale wanaoendelea kupatiwa matibabu ya kuchuja damu wasikate tamaa, kwa sababu ugonjwa huo unatibika.

“Mimi niliyesimama mbele yenu ni ushuhuda kwamba ugonjwa wa figo unatibika tena hapa nchini, naiomba Serikali iendelee kuwezesha Muhimbili izidi kufanya upasuaji huu.

“Nawasihi ndugu wa wagonjwa nao wasikate tamaa, wajitokeze kuwachangia figo ndugu zao wenye uhitaji kama ambavyo ndugu yangu amefanya na wote sisi ni wazima,” alisema.

Kwa upande wake, Batholomayo, alisema anamshukuru Mungu kufanikisha upasuaji huo kwenda kwa mafanikio makubwa.

“Nasikia furaha, sina mengi ya kusema zaidi ya kumshukuru Mungu na madaktari wetu kwa hatua hii tuliyofikia,” alisema.

Bingwa wa Magonjwa ya Figo wa MNH, Dk. Jaqueline Shoo, alisema walitumia zaidi ya saa nne kufanikisha upasuaji huo wa kihistoria.

“Hili ni jambo jema, tunamshukuru Mungu mgonjwa wetu anaendelea vizuri, anakwenda haja ndogo kama kawaida, anakula vizuri na kila kitu ana uwezo wa kufanya kama watu wengine,” alisema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa MNH, Aminiel Aligaesha, alisema upasuaji huo umegharimu Sh milioni 21.

“Matibabu hayo yamegharamiwa na Serikali, iwapo mgonjwa huyu angepelekwa nje ya nchi tungelipa takriban shilingi milioni 80 hadi 100,” alisema.

Einhard Mwingira, ambaye ni baba mdogo wa Priscer, aliiomba Serikali kumpa uhamisho wa kuja kuishi Dar es Salaam ili aweze kufuatiliwa kwa ukaribu.

“Ni mwalimu anaishi Morogoro, ameolewa, naomba ikiwa inawezekana pia aweze kubadilishwa kazi anayoifanya kwa sababu ya kuepuka lile vumbi la chaki na  akija Dar es Salaam itakuwa rahisi kufuatiliwa kwa ukaribu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles