29.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Aliyelipuliwa na JPM kortini

  • Ni bosi Takukuru, adaiwa kuchukua bilioni 1.6/- za wafanyakazi kwa ahadi ya kuwauzia viwanja

PATRICIA KIMELEMETA Na GRACE SHITUNDU-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthumu Mansoor, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 8 yakiwamo ya kughushi, uhujumu uchumi, kutakatisha na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh bilioni 1.4 kutoka kwa watumishi wa Takukuru    kwa ahadi ya kuwauzia viwanja.

Hatua ya kumfikisha mahakamani Kulthumu, imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kutaka kujua hatua alizochukuliwa mtuhumiwa huyo.

Juzi akiwa anapokea ripoti ya mwaka ya Takukuru sambamba na kumwapisha aliyekuwa Mkurugenzi wa Takukuru kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola, Rais Magufuli, alisema anashangazwa na Taasisi hiyo kutomchukulia hatua Kulthumu huku wafanyakazi waliodhulumiwa wakilalamika pembeni.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mwandamizi, Kelvin Mhina, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai kuwa tarehe tofauti Januari 2013 na Mei 2018, mshtakiwa huyo alijipatia fedha kutoka kwa wafanyakazi wenzake sita.

Alidai mshtakiwa huyo alighushi barua ya ofa ya tarehe 13, Agosti 2003 kwa madhumuni ya kuonyesha kuwa barua hiyo imetolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo huku akijua kuwa si kweli.

Alidai katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa kati ya Januari 2012 na Mei 2017, huko Upanga ndani ya Wilaya ya Ilala, mshtakiwa kwa kudanganya, alijipatia jumla ya Sh milioni 32.2 kutoka kwa watu sita tofauti kama malipo ya viwanja tofauti vilivyoko Wilaya ya Bagamoyo katika Kijiji cha Ukuni ambapo alijifanya kuwa yeye ni mmiliki wa viwanja hivyo huku akijua kuwa si kweli.

Wakili Wankyo, alidai kuwa mshtakiwa huyo alijipatia fedha hizo kutoka kwa Alex Mavika (milioni 5.2), Wakati Katondo (milioni 3), Gogo James, (milioni 5), Ekwabi Majungu (milioni 7), John Amos (milioni 7) na Rose Anatory, (milioni 5), ambao wote ni wafanyakazi wa Takukuru.

Katika shtaka la mwisho anadaiwa kuwa kati ya Januari 2013 na Mei 2018 huko Upanga, mshtakiwa alijipatia kiasi cha Sh 1,477,243,000 wakati akijua kuwa  fedha hizo ni haramu na kwamba limetokana na zao la kosa tangulizi la kughushi.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Wakili Wankyo alidai kuwa upelelezi katika kesi hiyo bado unaendelea na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kutokana na hayo, Hakimu Mhina, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 12, 2019 kwa ajili ya kutajwa.

Juzi wakati anamwapisha Balozi wa Cuba, Valentino Mlowola pamoja na kupokea ripoti ya Taasisi hiyo, Rais Dk. Magufuli, alimtaja mshtakiwa huyo akisema:

“Nashangaa kuona yule Mkurugenzi wa Takukuru aliyechukua fedha na kuwauzia viwanja hewa bado hajafikishwa mahakamani mpaka sasa, wafanyakazi wanashindwa kumdai kwa sababu ni bosi wao, wanaumia, wanalalamika pembeni na aliwadanganya kama ana viwanja kule Bagamoyo,” alisema Magufuli.

Jana kabla ya kufikishwa mahakamani, akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema tayari uchunguzi wa suala hilo umekamilika na wamemfikisha Kulthumu mahakamani kwa kosa la kughushi na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu kinyume na vifungu vya sheria, vifungu namba 302, 333, 335 (a) na 337 vya sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 pitio la mwaka 2002.

Alisema Kulthumu anadaiwa kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia fedha taslimu kwa njia ya udanganyifu zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kutoka kwa watumishi wa Takukuru kwa ahadi ya kuwauzia viwanja vilivyopo katika eneo alilodai kuwa analimiliki kihalali huko Nzole Ukuni Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

 “Sasa tuhuma zinazomkabili ni kama ifuatavyo, mnamo mwaka 2012 akiwa mwajiriwa wa Takukuru kwa cheo cha Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, aliwajulisha watumishi wa Takukuru akidai kwamba analo eneo kubwa la ardhi analolimiliki kihalali katika eneo la Bagamoyo mkoani Pwani na kwamba anataka kuwauzia viwanja watumishi kwa utaratibu wa kulipia fedha taslimu au kulipa kidogo kidogo kwa wale watakaohitaji.

“Viwanja hivyo ambavyo vilikuwa vya  ukubwa tofauti tofauti, vilikuwa vikiuzwa kwa thamani kati ya shilingi milioni tano na milioni saba kwa mtumishi binafsi kwa utaratibu wa kulipia fedha taslimu au kidogo kidogo kwa awamu.”

Aliongeza kusema: “Watumishi wa Takukuru walikubaliana na utaratibu huo  na walijiorodhesha kununua viwanja hivyo wao pamoja na ndugu zao na kumlipa Kulthumu fedha kwa utaratibu waliokubaliana.”

Brigedia Jenerali Mbungo alieleza kwamba, baada ya makubaliano hayo, watumishi waliokamilisha malipo yao walianza kuona dalili za kudanganywa baada ya kutokabidhiwa hati za viwanja wala nyaraka yoyote inayoonyesha umiliki halali wa kiwanja au viwanja walivyokuwa wakinunua na walipofuatilia na kuuliza, Kulthumu alisema viwanja hivyo vina mgogoro ambao upo mahakamani.

“Baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi dhidi ya mtuhumiwa Kulthumu, Takukuru na mamlaka nyingine tulifanya uchunguzi na kubaini kwamba viwanja vilivyoahidiwa kuuzwa vilikuwa ni zaidi ya 300.

“Fedha alizokwisha kulipwa Kulthumu Mansoor na watumishi kwa ajili ya kulipia viwanja hivyo ni zaidi ya shilingi bilioni 1.4, pia mtuhumiwa alijipatia fedha nyingine zaidi ya shilingi milioni 200 ambazo alilipwa na watumishi kama gharama ya kulipia hati na nyaraka nyingine za umiliki hivyo ukijumlisha unapata ni bilioni 1.6,” alisema.

Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo alisema pia walibaini fedha hizo milioni 200 hazikuwahi kuwasilishwa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya hati na wala tozo mbalimbali za ardhi.

Alisema pia Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi imethibitisha kwamba Kulthumu si mmiliki halali wa viwanja hivyo vilivyokuwa katika mazungumzo au mapatano ya kuuzwa.

“Viwanja vilivyokuwa vikizungumziwa kama vinauzwa havikuwa vya Kulthumu  na kwamba hakuwa na umiliki wowote wa viwanja hivyo na nyaraka alizokuwa akidai kuwa zinahalalisha umiliki wake zote zilikuwa ni za kughushi,” alisema.

Alisema hatua zilizochukuliwa baada ya uchunguzi huo, Takukuru ilimsimamisha kazi rasmi tangu Machi 8, mwaka 2018 kabla ya jana kumfikisha mahakamani kwa makosa hayo.

Alieleza kwamba, Kulthumu alijiunga na Takukuru na kuwa katika nafasi ya Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini Oktoba 2009, akiwa amehamishwa kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria.

Aidha, Brigedia Jenerali Mbungo, aliwashauri wananchi kubadilisha mwelekeo na staili ya maisha kwa kuwa zama zimebadilika.

“Serikali ya Awamu ya Tano imejibainisha wazi kabisa kwamba haitavumilia vitendo vyovyote vinavyonyang’anya haki ya mtu yeyote, ikiwemo vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa fedha, ujanja ujanja unaofanywa na baadhi ya watumishi katika kupata mali ambazo hawastahili, kuwa na malimbikizo ya mali ambayo hayana maelezo yoyote.

“Wananchi waelewe zama zimebadilika, waelewe zama za ujanja ujanja hazipo tena, watumishi wa Serikali, watumishi wa mashirika ya umma na watu wengine wanaofanyakazi kwenye taasisi binafsi, mwelekeo sasa ni kubadilisha gia, ni kuwa waaminifu, kujibidisha katika kufanya kazi kupata vipato halali na kusukuma mbele maendeleo ya nchi na kuhakikisha nchi inapata kodi,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles