HATIMAYE Mkurugenzi wa ufundi wa timu ya Al Ahly, Syed Abdul Hafeez anatarajia kutua Aprili 3 nchini ili kusuka mipango ya ushindi na kuandaa kambi ya kufikia timu hiyo kabla ya kuvaana na Yanga kwenye hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Aprili 9 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hatua hiyo imekuja baada ya uongozi wa timu hiyo kukataa hoteli tano zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili kufikia.
Hafeez atakuwa na jukumu la kusuka mipango yote inayohusiana na ushindi, kabla ya timu hiyo haijatua kuvaana na Yanga Aprili 9.
Kabla ya kutua nchini Al Ahly inatarajia kucheza dhidi ya timu ya Polisi, inayoshiriki Ligi Kuu nchini Misri na baada ya kurejea timu hiyo itavaana na ENPPI na baadaye kurudiana na Yanga Aprili 20 mwaka huu.
Ushindi ulioipata timu hiyo hivi karibuni dhidi ya Dirout kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Mabingwa nchini Misri, huenda ikawa chachu ya kufanya vizuri kwenye mchezo wake dhidi ya Yanga.