27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

AJIRA ZA TRA ZAONYESHA UKUBWA TATIZO LA AJIRA

Na EVANS MAGEGE

KITENDO cha watu zaidi ya 56,000 kujitokeza kuwania nafasi 400 za ajira zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), kinaonyesha namna ambavyo kwa sasa kuna wasomi wengi mtaani wasio na ajira.

Licha ya kwamba baadhi ya waliojitokeza kusaka nafasi hizo wengine yawezekana kabisa wana ajira sehemu nyingine, lakini wanataka kubadilisha aina ya kazi, kwa vyovyote vile, wasio kabisa kwenye kundi hilo ni wengi zaidi.

Katika kile kinachoonyesha kwamba, pamoja na uhitaji huo bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kati ya idadi hiyo iliyojitokeza kutaka nafasi hizo, 26,000 hawakufika hata kwenye hatua ya usaili, kwani walioitwa ni 30,000 pekee.

Hali kama hiyo pia ilijitokeza Julai 2014, ambapo vijana 6,740 walifanya usaili wa kuwania nafasi za kazi 47 zilizokuwa zimetangazwa na Shirika za Viwango Tanzania (TBS).

Pia Juni mwaka huo huo, vijana 10,000 walifanya usaili wa kuwania nafasi za kazi 70 za Idara ya Uhamiaji.

Hali hiyo inafanya kuwapo na mitizamo miwili, wa kwanza ukiwa ni uwepo wa wahitimu wengi wa elimu ya juu wasio na sifa za kuingia kwenye ajira na wa pili ukiwa ni kwamba, elimu ya kujiajiri ni muhimu zaidi, kwani panapokuwa na nafasi chache na wahitaji wakiwa wengi, mwajiri anatumia kila kigezo kuhakikisha anapata anaowahitaji, huku wengi wakibaki.

Utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi Tanzania Bara uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2014, ulionyesha Watanzania milioni 2.3 hawana ajira. Kiwango hicho ni sawa na asilimia 10.3 ya nguvu kazi ya Taifa.

Kwa mujibu wa utafiti huo, watu wengi wasio na ajira wanatumia muda mwingi kusaka ajira.

Utafiti huo unasema, kiwango cha ukosefu wa ajira kimeongezeka kutoka asilimia 17.9 mwaka 2006 hadi kufikia asilimia 32.5 mwaka 2014.

Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini nchini (REPOA), Dk. Lucas Katera, amewahi kukaririwa na gazeti moja (si MTANZANIA) akikiri uwapo wa tatizo la ukosefu wa ajira, hususan wanaomaliza elimu ya juu.

Dk. Katera alisema kwa sasa idadi ya watu wasio na ajira ni asilimia 12 ya idadi ya Watanzania wote wanaokaribia  kufika milioni 50.

Alisema asilimia 57 ya Watanzania wana uwezo wa kufanya kazi na jumla yao ni milioni 26.

Dk. Katera alisema sekta ya kilimo, ambayo kwa sasa inaajiri asilimia 70 ya nguvu kazi, inachangia pato la Taifa kwa asilimia 25, lakini inaonekana bado haina mvuto kwa vijana wanaomaliza elimu ya juu.

Alizitaja sekta zinazokuwa kwa kazi kama vile huduma za jamii, benki na bima, zinachangia asilimia 50 ya Pato la Taifa, lakini bado hazina uwezo wa kuzalisha ajira nyingi.

Alisema sababu nyingine ni kutokuwapo kwa uwiano mzuri wa kile kinachohitajika kwenye soko la ajira na elimu inayotolea vyuoni.

Alisema vyuo vinazalisha wahitimu wengi, hali inayofanya aina ya elimu inayotolewa na vyuo kukinzana na mahitaji ya soko ajira lilivyo sasa.

“Ni kweli watu wengi hawana kazi, lakini ukitangaza sasa nafazi za kazi watu watakaokuja utashangaa na utajiuliza hivi kweli hawa watu wanahitaji aina hii ya kazi? Inaonekana hakuna uwiano mzuri wa kilichofundishwa na soko la ajira,” alisema Dk. Katera.

Wakati hali ikiwa hivyo, Aprili 22 mwaka jana, katika Bunge la Bajeti, Waziri Mkuu  Kassim Majaliwa alisema ukosefu wa ajira kwa vijana nchini umepungua kwa asilimia 2.5 na kwamba Serikali itaendeleza juhudi za kuvutia uwekezaji ili kupunguza zaidi kiwango hicho.

“Utafiti wa hali ya ajira nchini wa mwaka 2014 unaonyesha ukosefu wa ajira umepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi 10.3 mwaka 2014. Ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014,” alisema.

Alisema changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni vijana kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza programu ya miaka mitano ya kukuza ujuzi nchini.

“Programu hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia tatu ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya watu wenye kiwango cha ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 54,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles