Patricia Kimelemeta na Mauli Muyenjwa, Dar es Salaam
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefuta ajira 200 za uhamiaji zikiwamo 28 kutoka Zanzibar kutokana na madai mbalimbali yakiwamo ya watumishi wa idara hiyo kuajiri ndugu na jamaa zao.
“Tumefuta ajira za watu 200 zikiwamo 28 kutoka Zanzibar za idara ya uhamiaji kwa nafasi ya konstebo na koplo ambazo zilizotangazwa na vyombo vya habari nchini,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbaraka Abdulwakil, Dar es Salaam jana.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kamati ndogo ya watu watano iliyoundwa kuchunguza mchakato wa ajira hizo kuchunguza tuhuma hizo na kutoa ushauri wa hatua zitakazochukuliwa, kugundua upungufu mkubwa uliokuwapo.
Mbaraka alisema kamati hiyo ilibaini kuwa matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari yalikuwa ya jumla na hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha nne na sita.
Mengine yaliyobainika ni kuwa baadhi ya watu waliofanyiwa usaili na kupata alama za juu za ufaulu kwenye mitihani yao hawakuitwa kwenye matangazo ya kazi wala kazini na hawajapewa sababu yoyote yao kutoitwa.
Vilevile, baadhi ya waombaji wa kazi wenye umri zaidi ya uliotajwa kwenye matangazo ya kazi; 25 kwa konstebo na miaka 30 kwa koplo walisainiwa na kuitwa kazini, alisema.
Alisema kamati ilithibitisha kuwa wasailiwa waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa ndugu na jamaa wa watumishi wa idara hiyo.
Katibu mkuu alisema wizara imeamua kufuta ajira hizo, kuwaita na kuwahoji watumishi walioajiri watoto, ndugu na jamaa zao waweze kuchukuliwa hatua za sheria.
“Unajua huwezi kumwita mwanao kwenye usaili lazima utampa ajira hata kama ameshindwa kujieleza.
Hali hiyo ni sawa na kumsimamia mtihani wa taifa mwanao halafu unamsahihisha lazima utampa alama za juu aonekane amefaulu hata kama ameshindwa mtihani huo,”alisema.
Alisema mchakato wa ajira hizo utatangazwa upya hivi karibuni na utasimamiwa na wizara yenyewe ili kuwapata watu wenye sifa zinazotakiwa.
Serikali ilitangaza nafasi za kazi za konstebo na koplo wa idara ya uhamiaji Februari 7 mwaka huu, na baada ya tangazo hilo maombi 15,707 yalipokelewa huku waombaji 1005 waliitwa kwenye usaili.
Baada ya kukamilika usaili yalijitokeza malalamiko mengi yakiwamo ya watumishi wa idara hiyo kuajiri watoto, ndugu na jamaa zao.