22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 14, 2024

Contact us: [email protected]

Ajira 200 Uhamiaji zafutwa rasmi

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbaraka  Abdulwakil
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbaraka Abdulwakil

Patricia Kimelemeta na Mauli Muyenjwa, Dar es Salaam

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefuta ajira  200 za uhamiaji zikiwamo  28 kutoka Zanzibar kutokana na madai mbalimbali yakiwamo ya watumishi wa idara hiyo kuajiri   ndugu na jamaa zao.

“Tumefuta ajira za watu 200 zikiwamo 28 kutoka Zanzibar za idara ya uhamiaji kwa nafasi ya konstebo na koplo ambazo zilizotangazwa na vyombo   vya habari nchini,” alisema Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbaraka  Abdulwakil, Dar es Salaam jana.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kamati ndogo ya watu watano iliyoundwa kuchunguza mchakato wa ajira hizo kuchunguza tuhuma hizo na kutoa ushauri wa hatua zitakazochukuliwa, kugundua upungufu mkubwa uliokuwapo.

Mbaraka alisema kamati hiyo ilibaini kuwa matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari yalikuwa ya jumla na  hayakuainisha  viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha nne na sita.

Mengine yaliyobainika ni  kuwa baadhi ya watu  waliofanyiwa usaili   na kupata alama za juu za ufaulu kwenye mitihani yao hawakuitwa kwenye matangazo ya kazi wala kazini na   hawajapewa sababu yoyote yao kutoitwa.

Vilevile,  baadhi ya waombaji wa kazi wenye umri zaidi ya uliotajwa   kwenye matangazo ya kazi;  25 kwa   konstebo  na miaka 30 kwa koplo   walisainiwa na kuitwa kazini, alisema.

Alisema kamati ilithibitisha  kuwa wasailiwa waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa  ndugu na jamaa wa watumishi wa idara hiyo.

Katibu mkuu alisema   wizara imeamua kufuta ajira hizo,   kuwaita na kuwahoji watumishi walioajiri watoto, ndugu na jamaa zao  waweze kuchukuliwa hatua za sheria.

“Unajua huwezi kumwita mwanao kwenye usaili lazima utampa ajira hata kama ameshindwa kujieleza.

Hali hiyo ni sawa na kumsimamia mtihani wa taifa mwanao halafu unamsahihisha lazima utampa alama za juu  aonekane amefaulu hata kama ameshindwa mtihani huo,”alisema.

Alisema   mchakato wa ajira hizo utatangazwa upya hivi karibuni na utasimamiwa na wizara yenyewe ili kuwapata watu wenye sifa zinazotakiwa.

Serikali ilitangaza nafasi za kazi za konstebo na koplo wa idara ya uhamiaji Februari 7 mwaka huu, na baada ya tangazo hilo   maombi 15,707 yalipokelewa huku waombaji 1005 waliitwa kwenye usaili.

Baada ya kukamilika   usaili yalijitokeza malalamiko mengi yakiwamo ya watumishi wa idara hiyo kuajiri watoto, ndugu na jamaa zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles