Na IBRAHIM YASSIN, MBOZI
MKAZI wa Kijiji cha Kokoto katika Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Daud Haonga (70), amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia shuka kwa madai ya kuugua muda mrefu bila kupona.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakutaka majina yao yatajwe, Haonga alijinyonga wakati ndugu zake aliokuwa akiishi nao wakiwa kwenye shughuli zao.
“Ndugu wa Haonga waliporudi kutoka kwenye shughuli zao, walipoingia ndani walimkuta akiwa ananing’inia juu, huku akiwa amejipiga kitanzi kwa kutumia shuka na akaacha ujumbe uliosomeka; ‘Nimeamua kujiua ili nipumzike baada ya kuugua muda mrefu’,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.
Baada ya tukio hilo, Serikali ya Kijiji ilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi waliofika na kuuchukua mwili wa marehemu.
Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Mathius Nyange, alisema walipopata taarifa hiyo walikwenda kuchukua mwili huo na kuupeleka hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
“Chanzo cha Haonga kujiua ilitokana na kuugua mara kwa mara kwa muda mrefu, na alisubiri siku hiyo watu waondoke maeneo ya karibu na nyumba yake ndipo alipoingia ndani na kuchukua maamuzi hayo magumu.
“Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa Haonga amekufa kwa kujinyonga na hakuna aliyekamatwa kuhusiana na kifo hicho,” alisema Kamanda Nyange.
Katika tukio jingine, Kamanda Nyange alisema Mkazi wa Mtaa wa Ilembo wilayani Mbozi, Kalinga Andulile (43), amekutwa ameuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali shingoni na watu wasiofahamika.
Alisema Andulile alikutwa na umauti akiwa lindoni katika baa ya Gs na wauaji waliiba pikipiki mbili zenye thamani ya Sh milioni 3.7.
Kamanda Nyange alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuwasaka wauaji hao.