Na HASSAN DAUDI
Milaois Murphy ni mwanamke aishie katika Jiji la Dublin, Jamhuri ya Ireland. Mwanamke huyu alifikia hatua ya kujifungua mtoto huku akiwa hajui kama alibeba ujauzito.
Hiyo inaweza kumwacha hoi kila atakayeisikia, lakini ni ukweli kabisa na imemtokea Milaois ambaye ameisimulia katika mahojiano yake na kipindi cha ‘The Rotunda’ kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha RTE cha Ireland.
Milaois (18), anasema alianza kunyimwa usingizi na maumivu makali ya mgongo ambayo kwa mujibu wa maelezo aliyopewa na daktari wake aitwaye Victoria, yalitokana na kidole tumbo (appendix), tatizo lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
“Kuna kipindi nilisikia kabisa kitu kinapiga tumboni lakini kwa sababu sikuwahi kushika ujauzito, sikufikiria kuwa ni mtoto. Nilidhani labda ni upepo au kitu kingine,” anasema.
Anasimulia kuwa siku moja akiwa hana hili wala lile katika shughuli zake za jikoni, alihisi maumivu makali na ghafla kilichofuata ni kuliita gari la wagonjwa (ambulance) ili limpeleke hospitali.
“Usiku ule, nilikuwa natapika na nilimwambia mama kuwa nataka kwenda hospitali. Tulidhani ni tatizo langu la kidole tumbo…Si mimi wala mama, hakuna kati yetu aliyekuwa akifikiria kuhusu mimba,” anasema msichana huyo anayeishi kwao licha ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na James Mulligan.
Hata hivyo, wakati wakisubiri gari hilo, ghafla Milaois alihisi mabadiliko, ikiwamo kuhisi ongezeko la shinikizo la damu (presha) na kutokwa na maji mengi ukeni.
Haikuchukua zaidi ya dakika tano kabla ya kujifungua mtoto wa kike.
“Yaani sikuamini, nilishtushwa mno. Ujauzito? Ni kitu ambacho sikukifikiria kabisa kichwani kwangu. Hakukuwa na dalili zozote,” anasema Milaois.
Akisimulia alivyokwenda katika nyumba hiyo na kukuta Milaois ameshajifungua, Adrienne Foran, Mtaalamu wa Afya ya Uzazi katika Hospitali ya Rotunda iliyopo mjini Dublin, Adrienne Foran anasema:
“Nilikuta ana takribani dakika 20 baada ya kuzaliwa na hakuwa na kasi ya mapigo ya moyo…Mtoto alikuwa na umbo dogo.”
Kwa bahati mbaya, baadaye madaktari walisema kichanga hicho ni njiti, kwamba kimekaa tumboni kwa wiki 26 pekee (miezi sita na nusu) na si miezi tisa kama ilivyo kawaida. Pia, tofauti na watoto wengine wanapozaliwa, Harper alikuwa na uzito mdogo (gramu 458).
Hiyo ilisababisha mtoto huyo anayeitwa Harper kubaki chini ya uangalizi maalumu wa madaktari bingwa kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu.
Mbali na hilo la uzito, pia sababu kubwa ya madaktari kutaka kubaki na mtoto huyo kwa matibabu zaidi ni tatizo lake la mfumo wa upumuaji.
Harper ana miezi mitano kwa sasa na mbali ya mama yake, Milaois, aliyelazimika kusitisha masomo ili kuhakikisha anakuwa naye karibu, anaishi na baba yake, Mulligan.
Afya ya mtoto huyo nayo imeonekana kuimarika kwa kiasi kikubwa kwani licha ya kuzaliwa akiwa na gramu 485, hivi sasa ana uzito wa kilo 3.6.