25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

AJALI YAUA WATU 26, MAGUFULI AWALILIA

NA GUSTAPHU HAULE-PWANI


Ni huzuni. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya watu 26 kufariki dunia na wengine tisa kujeruhiwa baada ya magari mawili kugongana uso kwa uso, eneo la Kitonga, Kata ya Mwarusembe wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa tatu usiku ikihusisha gari dogo la abiria aina ya Toyota Hiace na lori yaliyogongana uso kwa uso katika eneo hilo na kusababisha vifo na majeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia MTANZANIA, Toyota Hiace ilikuwa ikitoka Dar es Salaam kwenda Kimanzichana wilayani Mkuranga, huku lori likitoka mkoani Lindi  kwenda Dar es Salaam.

Akizungumza jana na MTANZANIA, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkuranga, Dk. Stephen Mwandambo alikiri kupokea maiti 25 zilizotokana na ajali hiyo.

Alisema majeruhi wote walikuwa na hali mbaya hivyo walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili lakini wakiwa njiani, mmoja wa majeruhi alifariki dunia.

“Jana usiku (juzi), nilipokea maiti 25 na majeruhi 10 wa ajali ya magari kugongana eneo la Kitonga, majeruhi walikuwa na hali mbaya tulilazimika kuwakimbiza Muhimbili, kwa bahati mmoja alipoteza maisha tukiwa njiani na kufanya idadi ya waliokufa kufikia 26,” alisema Dk. Mwandambo.

Alisema majeruhi tisa wanaendelea kupatiwa matibabu na maiti zimehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.

Aliwataja waliofariki na kutambuliwa majina yao ni 17 kati ya 26 ambao ni Selemani Guli (36), mkazi wa Kongowe, Modesta Sheleli (24) mkazi wa Vianzi, Doreen Selemani Seleli (5) na Sheila Hamad Mkuba (8) mkazi wa Vianzi.

Wengine ni Mariam Hussein Sadik (15 ) mkazi wa Mwarusembe, Nassoro Hamis (48) mkazi wa Jaribu Mpaka, Asha Athumani (24) mkazi wa Songosongo na Nasma Athuman (22) mkazi wa Songosongo.

Aliwataja pia Mwanahawa Athuman (52), Mohammed Saidi (25) mkazi wa Njopeka,  Mwajabu Jongo (20) mkazi wa Njopeka, Mwarami Mbunju (37) mkazi wa Mkamba na Abisaalom Uloga (25) mkazi wa Kimanzichana.

Mbali na hao, wengine waliopoteza maisha ni Kijongo Kibwana Jongo (26 ) mkazi wa Jaribu Mpakani na Recho Japhet (16), Mariam Selemani (36) wakazi wa Mbagala  na Melania Kapatwa (38) mkazi wa Jaribu Mpakani.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Kibiti, Mohamed Likwata alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.

Alisema uchumguzi wa ajali hiyo unaendelea.

 

JPM

Wakati huo huo, Rais Dk. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Greson Msigwa ilisema Rais Magufuli amesikitishwa na ajali hiyo.

“Nimesikitishwa na taarifa ya vifo vya watu 26 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea Mkuranga mkoani Pwani, tumepoteza idadi kubwa ya Watanzania wenzetu na nguvu kazi yaTaifa.

“Naungana na wafiwa wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao na watu waliowategemea,” ilisema taarifa hiyo.

Rais Dk. Magufuli amemtaka Mhandisi Ndikilo kumfikishia salamu za pole kwa familia za marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo hivyo na pia amevitaka vyombo vya usalama   kuchunguza chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua zinazostahili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles