Na RAMADHAN HASSAN–DODOMA
ZAIDI ya abiria 150 wamenusurika kifo huku 32 wakijeruhiwa baada ya gari aina ya Isuzu kuigonga treni iliyokuwa ikitokea Kigoma kuelekea Jijini Dar es salaam katika eneo la Hazina jijini hapa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema treni hiyo ilikuwa na mabehewa 14 ambapo mawili yalianguka na kusababisha ajali hiyo.
Alisema ajali hiyo imehusisha gari lenye namba za usajili T 860 APW aina ya Isuzu huku akitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa gari kutochukua tahadhari alipokuwa akivuka makutano ya reli.
Alisema mara baada ya gari hilo kuzima, dereva wake Hamisi Salum (49), Mkazi wa Nkuhungu jijini Dodoma, aliruka na kukimbilia na baadaye kujisalimisha polisi.
Alisema treni hiyo ilikuwa ikitokea Kigoma kupitia Mwanza na Mpanda kuelekea Dar es salaam ikiwa na behewa tisa za daraja la tatu, mbili daraja la kwanza, mgahawa mmoja, behewa la vifurushi na behewa la breki.
“Majeruhi 10 wamelazwa katika hospital ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wodi namba 1,16 na 17, wengine tumewaruhusu waendelee na safari,”alisema Kamanda Muroto
Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Abul Pumzi, alisema majeruhi wa ajali hiyo wanaendelea kupata matibabu katika Hospitali hiyo.