26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji mwanafunzi Scolastica

Na MWANDISHI WETU

-MOSHI

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, imemuhukumu kunyongwa hadi kufa aliyekuwa mlinzi wa Shule ya Scolastica mkoani Kilimanjaro, Hamis Chacha kwa kosa la kumuua kwa kukusudia aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo, Humprey Makundi.

Pia imemuhukumu mmiliki wa shule hiyo, Edward  Shayo na aliyekuwa mwalimu wa nidhamu, Labani Nabiswa kifungo cha miaka minne jela kila mmoja kwa kosa la kuficha ukweli wa mauaji hayo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Firmin Matogolo baada ya kumtia hatiani Chacha kwa kumuua kwa kukusudia Humprey ambaye alikuwa akisoma kidato cha pili katika shule hiyo.

Humprey aliuawa Novemba 6 mwaka 2017 na baadaye mwili wake kutupwa katika Mto Ghona, takribani mita 300 kutoka shuleni.

Mwili wa mwanafunzi huyo baada ya kuokotwa ulizikwa na manispaa kabla ya kufukuliwa kwa amri ya mahakama na kufanyiwa uchunguzi.

Awali mchana jana, mahakama hiyo ilimtia hatiani Chacha kwa mauaji, Shayo na Nabiswa kwa kosa dogo la kushiriki jinai.

Baada ya kuwatia hatiani, mahakama ilihairishwa kwa dakika 30 ili kuwawezesha mawakili wa washtakiwa kutoa maombi yao kabla ya jaji kutoa adhabu.

Kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Firmin Matogolo, ilianza Aprili 2 kusikilizwa kwa siku 11 na kuahirishwa Aprili 16 hadi Aprili 29.

Vielelezo vilivyopokewa na mahakama ni pamoja na panga linalodaiwa kutumika katika mauaji hayo, ripoti ya uchunguzi wa kifo na ya vinasaba (DNA).

Ripoti ya DNA ilitolewa na shahidi wa 12, mkemia wa Serikali, Hadija Mwema, ikieleza sampuli zilizochukuliwa kwenye mwili wa Humphery zilioana na zile za baba yake, Jackson Makundi na mama yake Joyce.

Vielelezo vingine ni ripoti ya mawasiliano ya simu zinazodaiwa za washtakiwa pamoja na maelezo ya ungamo ya mshtakiwa Chacha anayodaiwa kuyatoa kwa mlinzi wa amani, Novemba 20, 2017.

Pia simu za washtakiwa zilipokewa kama vielelezo. Kabla ya kupokewa kwa maelezo hayo, mahakama iliingia katika hatua ya kesi ndani ya kesi ili kujiridhisha kama uchukuaji wake ulifuata sheria na iwapo mshtakiwa aliyatoa kwa hiari.

Kati ya waliotoa ushahidi kwenye kesi hiyo, ni baba wa marehemu, Makundi, ambaye aliieleza mahakama namna alivyoutambua mwili wa mwanaye baada ya kufukuliwa.

Shahidi huyo alidai kuwa mmoja wa wanafunzi aliyekuwa akisoma na mwanaye, alimsisitiza afuatilie tetesi kuwa kuna mwanafunzi alipigwa na kuumizwa nyuma ya ukuta wa shule.

Akitoa ushahidi wake kama shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Makundi alidai Novemba 17, 2017 walifanikiwa kupata amri ya mahakama ya kuufukua mwili huo ukiwa umekaa kaburini kwa siku sita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles