27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Aguero aipeleka Argentina robo fainali

RIO, BRAZIL

WASHAMBULIAJI wa timu ya taifa Argentina, Sergio Aguero na Lautaro Martinez, usiku wa kuamkia jana waliibeba timu hiyo na kuipeleka robo fainali kwenye michuano ya Copa America nchini Brazil.

Argentina ilifanikiwa kushinda mabao 2-0 dhidi ya wageni waalikwa Qatar na wageni hao wakaungana na Paraguay kuyaaga mashindano.

Mchezo huo ulikuwa wa mwisho katika hatua ya makundi, ambapo Argentina ikiwa chini ya nahodha wao Lionel Messi ilikuwa inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kujihakikishia inaingia hatua hiyo.

Timu hizo zilikuwa zinaunda kundi B, huku Colombia ikiwa ya kwanza kufuzu robo fainali kabla ya mchezo wao wa juzi, hivyo mtihani ulikuwa kwa Argentina na Paraguay ambaye kila mmoja alikuwa anahitaji kushinda mchezo wa mwisho.

Endapo Paraguay wangefanikiwa kushinda dhidi ya Colombia, basi wangefuzu robo fainali bila ya kujali matokeo ya Argentina kwa kuwa wangekuwa wamezidiwa pointi moja.

Argentina walikuwa na kila sababu ya kushinda mchezo huo dhidi ya Qatar kwa kuwa walitengeneza nafasi nyingi lakini walikosa bahati ya kufunga mabao mengi. Mbali na Aguero kufunga bao moja, lakini kuna nafasi ya wazi ambayo aliipoteza.

Kwa upande mwingine nahodha wao Messi, alionekana kuwa chini ya ulinzi wa Qatar ambao walihakikisha anatoka bila ya bao, lakini kulikuwa na nafasi ambayo aliipata ila shuti lake lilikwenda moja kwa moja na kugonga mwamba.

Kwa sasa Argentina wanatarajia kukutana na Venezuela kwenye mchezo wao wa robo fainali Ijumaa wiki hii ambapo mshindi moja kwa moja ataingia nusu fainali.

Messi amewatoa wasiwasi mashabiki wa Argentina kuelekea mchezo huo wa robo fainali huku akiwahakikishia kufanya vizuri na kuingia hatua ya nusu fainali.

“Tunashukuru kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali, kilichobaki ni kuufikilia mchezo unaofuata, tupo tayari na tunaamini tutafanya vizuri na kuingia hatua inayofuata,” alisema mchezaji huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles