29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 21, 2024

Contact us: [email protected]

AGENDA yawajengea uwezo wadau juu ya usimamizi wa taka hatarishi za betri chakavu

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Asasi isiyo ya kiserikali ya AGENDA kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Oeko-Institut ya Ujerumani kwa ufadhili wa Shirika la ushirikiano wa kimataifa la Ujerumani (GIZ) wameendesha warsha maalum ya siku moja inayoangazia namna bora ya usimamizi wa taka hatarishi zinazotokana na betri chakavu. Warsha hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikumi, Millenium Tower, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Meneja wa Uzingatiaji wa NEMC, Hamadi Taimuru, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, amesema kuwa lengo kuu la warsha ni kutoa mwongozo bora juu ya usimamizi wa betri chakavu ili kuepusha madhara kwa mazingira na afya ya jamii.

“Hii ni wiki ya kuchukua tahadhari dhidi ya uchafuzi unaotokana na betri chakavu. Warsha hii itakuwa ya siku mbili na tutaenda kutembelea viwanda vinavyojihusisha na urejelezaji wa betri chakavu. Ni matarajio yetu kwamba warsha hii itatoa uelekeo mzuri wa namna bora ya usimamizi wa taka hatarishi ili zisilete madhara kwa afya ya binadamu na mazingira,” alisema Taimuru.

Meneja wa Uzingatiaji wa NEMC, Hamadi Taimuru.

Aidha, Taimuru alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda vinavyojihusisha na urejelezaji wa betri chakavu kuhakikisha wanafanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kuanza shughuli hizo. Pia aliwasisitiza kupata vibali maalum kutoka NEMC na taasisi nyingine za serikali ili kuhakikisha mchakato wa urejelezaji unazingatia sheria, kanuni, na taratibu za Mazingira.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Taasisi ya AGENDA, Dora Swai, alisisitiza kuwa urejelezaji wa betri chakavu ni hatari sana endapo hautasimamiwa ipasavyo. “Madini yanayopatikana kwenye betri chakavu, hususani ‘lead,’ yana madhara makubwa kwa mazingira na afya ya binadamu, na yanaweza kusababisha magonjwa ya figo, ini, na ubongo,” amesema Swai.

Katibu Mtendaji wa Taasisi ya AGENDA, Dora Swai, akizungumza wakati wa warsha hiyo.

Mratibu wa Shughuli za Taasisi ya Wadau wa Urejelezaji Tanzania (TARA), Henry Kazula, aliwataka wadau wote kushiriki katika warsha mbalimbali ili kuongeza uelewa juu ya urejelezaji wa taka hatarishi. “Ni muhimu kwa taasisi na wadau wote kudhibiti athari zinazotokana na betri chakavu kwa jamii,” amesema Kazula.

Warsha hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Agenda kwa kushirikiana na NEMC na Taasisi ya OEKO kutoka Ujerumani. Miongoni mwa washiriki ni maafisa mazingira wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, OSHA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na wamiliki wa viwanda vinavyohusika na urejelezaji wa taka hatarishi.

Afisa Mwandamizi Mradi wa AGENDA, Silvana Mng’anya akiwasilisha mada wakati wa warsha hiyo.

Warsha hii inalenga kutoa maarifa na mbinu bora za kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na betri chakavu, hatua muhimu kwa afya ya jamii na uhifadhi wa mazingira nchini.

Sehemu ya washiriki wa warsha hiyo.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles