Na FERDNANDA MBAMILA -DAR ES SALAAM
TAASISI ya Huduma ya Afya Aga Khan Tanzania, inakusudia kujenga vituo 35 vya afya kila mkoa ifikapo mwaka 2020.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Rachel Mhando, alisema dhamira kubwa ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora, angalizi, nafuu na za kudumu kwa wote pasipo kujali tofauti za dini, chama, kabila na rangi.
“Mpango mkakati ni kwamba ifikapo Desemba, mwaka 2020 taasisi itakuwa imekwishakamilisha kufungua vituo 35 nchi nzima kwa kushirikiana na Serikali katika kutoa miongozo,” alisema.
Mbali na utoaji wa huduma ya afya, alisema hadi sasa imetoa fursa za kada mbalimbali za ajira 15 na kuchangia upatikanaji wa kazi za kitaalamu zikiwamo ugavi, wataalamu wa maabara, mafamasia, madaktari wenye viwango na weledi katika maeneo tofauti.
Alisema huu ni ukuaji wa uchumi mtambuko unaokwenda kujenga sekta ya uchumi kwa kupunguza kiwango cha utegemezi hasa ukizingatia katika uwekezaji kwa sababu unawapa vijana fursa za ajira.
“Ifikapo mwaka 2020, Watanzania takribani 625 watakuwa wamefunguliwa milango ya ajira nchi nzima kwa kupunguza ukuaji mkubwa wa kiuwiano katika kutegemeana na zaidi ya yote kuchochea vijana kupenda masomo ya sayansi ya afya kwa miaka ijayo,” alisema.