Na RAMADHAN HASSAN
-DODOMA
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Profesa Adelardus Kilangi, amesema ofisi yake bado inaendelea na mchakato wa kuipitia upya mikataba ya utafutaji na uchimbaji wa gesi, na kwamba wamegundua matatizo mbalimbali hadi sasa.
Alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2019/20, akijibu hoja ya Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM), ambaye wakati akichangia alimtaka kueleza suala la utoaji wa leseni kwa ajili ya kutafuta gesi.
“Nikuombe chonde chonde kwa kimakonde, kwanini hivi vibali vinachukua muda mrefu, tukuombe hayo majadiliano yakamilike ili vibali vitolewe, tangu Kalemani (Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani) umeingia haujatoa leseni hata moja, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu upo, naomba hili mnijibu,” alisema Ghasia.
Akimjibu, Profesa Kilangi alisema jambo hilo liliundiwa kamati na bado inaendelea kufuatilia upya mikataba hiyo ya gesi.
“Kama unafahamu Mheshimiwa Spika uliunda kamati ya kuangalia sekta ndogo, kamati ile ilikuja na taarifa yake na mapendekezo yako, mojawapo ya mapendekezo hayo ni kurejea hii mikataba ya gesi, kazi hiyo ikapewa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni kweli anaishughulikia.
“Tulianza kazi na zoezi la kuipitia na kuunda timu na tulipata wataalamu kutoka sekta mbalimbali, lakini ilitulazimu kwanza kuwajengea uwezo. Baada ya zoezi hilo lilifuata la kuipitia mikataba na hii timu imekaa kwa zaidi ya miezi miwli na imepitia mikataba yote 11.
“Tuligundua kwamba kuna kitu ambacho ni muhimu kukiangalia ‘Economic Financial Modeling’, hapo ni muhimu, hivyo tukaweka timu kwa mwezi mmoja, walichokifanya ilikuwa ni kuangalia ‘Economic Financial Modeling’, wakaona ni bora tuangalie kama nchi, sasa hilo zoezi la tatu timu hiyo inakutana tena tarehe 6 mwezi wa sita na itamaliza tarehe 25 mwezi wa sita,” alisema.
Profesa Kilangi alisema zoezi hilo limewasaidia kujua matatizo mengi ambayo yapo katika mikataba hiyo.
“Zoezi hili limetufanya tuelewe matatizo mengi, kikubwa kabisa litatufahamisha mambo mengi,” alisema.
Naye Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, aliijia juu Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kudai kwamba Serikali ya awamu ya tano hakuna kitu chochote ilichokifanya katika sekta ya nishati na hakuna mradi wowote wa umeme ilioukamilisha.
Akihitimisha mjadala wa wizara hiyo, Mgalu aliomba mwongozo kwa Spika, akitaka apewe majibu ni kwanini Kambi Rasmi ya Upinzani inapotosha kwamba hakuna mradi wowote ambao Serikali imeukamilisha.
“Tumesikiliza hotuba ya upinzani ilionesha hakuna jambo lililofanyika na hakuna mradi wowote uliokamilika, ningeomba mwongozo kwanini hotuba hii inapotosha.
“Kiwango cha uzalishaji umeme kimeongezeka, kwa sasa tuna megawati 300 za ziada, Serikali imetenda kazi nzuri.
“Kusema Serikali ya awamu ya tano haiiwezeshi REA hapana, kauli ya Kambi ya Upinzani sio kweli, pia Bunge limepotoshwa kwenye hasara ya Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania), kwani imekuwa ikipungua, ila tutaomba mwongozo, taarifa za upotoshaji ziondolewe katika ‘Hansard’ za Bunge,” alisema Mgalu.
Aidha alifafanua suala la kwamba Tanesco imekuwa ikijiendesha kwa hasara na kwamba ina madeni makubwa akidai kuwa kila mwaka madeni hayo yamekuwa yakipungua.
Alisema shirika hilo limekuwa likijiendesha vizuri kwa kutumia fedha za ndani ikiwa ni pamoja na kwenye uunganishaji wa gridi.
Kuhusu miradi ya REA, alisema Serikali itasimamia kuhakikisha inakamilika mwaka 2020.
“Mradi wa REA awamu ya tatu tumesikia mlivyotuelekeza, tutayafanyia kazi. Mradi huu wa REA awamu ya tatu pamoja na kwamba umechelewa, tunatambua wakandarasi ambao wanafanya vizuri na wanaofanya vibaya.
“Kazi ni ya miezi 24 na Juni 2020 ndio mradi utakamilika, tutahakikisha tunawasimamia na kukamilisha mpaka Desemba 2019 wawe wamekamilisha ili miezi sita itakayobaki iwe ya kuwaunganishia wateja umeme,” alisema.
Kuhusu mradi wa kufufua umeme wa Rufiji, Mgalu alisema Serikali itaendelea kuusimamia ikiamini kwamba utakuwa ni wenye tija kwa miaka ya baadae.
“Waheshimiwa wabunge, pamoja na michango yenu mizuri isiwe ya kupotosha, kwa sasa tunahitaji umeme mwingi, upo mradi mpya wa kuzalisha umeme wa megawati 3,000 mkoani Mtwara.
“Gesi hatuiachi, wimbo huo tunaimba ila tunaimba wimbo wa kwanza tupate wa bei rahisi.
“Ndani ya wizara hatutarudi nyuma, umeme ni biashara, miradi yote ikikamilika tutauza na umeme nje, hatutarudi nyuma, mwendo mdundo. Sisi wakazi wa Kibiti na Pwani tunajua fursa zitakazopatikana, tunatambua nia ya Rais ya kutaka bei ya umeme ipungue,” alisema.