23.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Kutupa mifuko ya plastiki faini Sh milioni 5

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema mabasi yatakayobainika kutupa uchafu wa plastiki yatatozwa faini ya hadi Sh milioni tano.

Akizungumza kwenye semina kwa waandishi wa habari kuhusu kanuni za usimamizi wa mazingira za kupiga marufuku mifuko ya plastiki jana, Mwanasheria wa NEMC, Manchare Heche, alisema uchafu huo wa plastiki ni ule wa ‘taka zilizosamehewa’.

Alisema taka hizo ni vifungashio vilivyotengenezwa viwandani kwa malighafi ya plastiki kwa ajili ya kuhifadhi vyakula kama korosho, mikate, maziwa na vingine vinavyofanana na hivyo.

 “Kama una gari lako umekula korosho halafu ukakamatwa umetupa kile kifungashio chake utatozwa Sh 200,000 na kama ni basi la abiria kampuni husika itatozwa Sh milioni tano.

“Hivyo tunatoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri vya binafsi na umma, wenye mabasi, meli na bajaji kuwa makini,” alisema Heche.

Akifafanua kuhusu makosa na adhabu nyingine, alisema kitendo cha kuzalisha au kuingiza nchini mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni 20 na isiyozidi Sh bilioni moja au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

Alisema kitendo cha kusafirisha nje mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni 20 au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

“Kitendo cha kuhifadhi au kusambaza mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni tano lakini isiyozidi Sh milioni 50 au kifungo kisichozidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.

“Kitendo cha kumiliki au kutumia mifuko ya plastiki adhabu yake ni faini isiyopungua Sh 30,000 lakini isiyozidi Sh 200,000 au kifungo kisichozidi siku saba au vyote kwa pamoja,” alisema.

MATUMIZI YANAYORUHUSIWA

Kulingana na kanuni hizo, vifungashio vya plastiki vinavyoruhusiwa ni vile vya huduma za afya, bidhaa za viwandani, sekta ya ujenzi, kilimo, vyakula au usafi na udhibiti wa taka na inasisitizwa kuwa viwango vyake visiwe chini ya 50.

Hata hivyo kanuni hizo zinaelekeza kuwa mhusika atakuwa na wajibu wa kuhakikisha taka za vifungashio hivyo  zinasimamiwa au kutupwa kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Taka Ngumu za mwaka 2009.

Naye Dk. Madoshi Makene, alisema kabla ya katazo hilo ulifanyika  utafiti wa ndani na kubaini kuna viwanda 94 vinavyojihusisha kutengeneza bidhaa za plastiki nchini huku zaidi ya 100 vikiwa ni viwanda bubu.

“Asilimia 80 ya viwanda vilivyokaguliwa havikuwa hata na cheti cha mazingira na kuna mikoa haina  viwanda. Wenye viwanda waingie kwenye teknolojia mpya watengeneze mifuko mbadala,” alisema Dk. Makene.

Meneja huyo alisema kila mkoa  utakuwa na watendaji wawili wa NEMC watakaosimamia hatua hiyo wakati katika Jiji la Dar es Salaam lenye kata 96 kutakuwa na mtendaji mmoja   kila kata.

MWONGOZO KWA WAKAGUZI

Mwongozo kwa wakaguzi na watekelezaji wa katazo la mifuko ya plastiki uliotolewa kwa halmashauri zote unaelekeza   ukaguzi utafanyika madukani, magengeni, sokoni, kwenye maduka makubwa, ghalani, viwandani na kwenye maeneo mengine zinakouzwa bidhaa.

“Wakati wote wa ukaguzi wajitambulishe na kuonyesha vitambulisho vyao kwa wahusika kwenye maeneo wanayoyakagua, hairuhusiwi kumsimamisha mtu na kumpekua au kupekua mizigo yake  kutafuta mifuko ya plastiki.

“Pia hairuhusiwi kuingia kwenye makazi ya watu au kusimamisha magari au vyombo vingine vya usafiri  kutafuta mifuko ya plastiki, iwapo vitasimamishwa kwa sababu nyinginezo na kukutwa na mifuko hiyo, adhabu stahiki itatolewa kwa wahusika na wataelekezwa mahali pa kupeleka shehena hiyo,” unaeleza mwongozo huo na kuongeza:

“Atayekutwa na kosa la kuendelea kuuza, kuhifadhi na kutumia mifuko hiyo ataelekezwa pa kuipeleka, atapigwa faini na atasainishwa fomu kukubali faini hiyo na atapewa muda wa kulipa.

“Atakapokataa kusaini au kushindwa kulipa katika muda aliopewa ndipo atafunguliwa mashitaka. Watakaotozwa na kulipa faini watapewa risiti za Serikali kwa malipo yao.”

WAZIRI WA MAZINGIRA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, alisema mifuko ya plastiki itakuwa ni malighafi kwa vile  tayari kuna viwanda vitatu vimejitokeza kutengeneza mabomba na madawati na kuwataka wenye shehena kubwa kwenda kuwauzia.

Alisema suala hilo lina masilahi ya  uchumi na wako watu ambao wamekuwa wakijaribu kufanya hatua hiyo isifanikiwe.

“Ni jambo gumu si jepesi kwa sababu limeingia katika maisha ya watu na shughuli zao za kila siku, ni kama zilivyo dawa za kulevya huwezi kuachana nazo.

“Lina masilahi ya  uchumi, kuna biashara kubwa ya wazalishaji wa ndani, waingizaji na katika biashara zilizokuwa zinaongoza kwa magendo hii pia ilikuwa mojawapo.

“Tumejaribu tangu mwaka 2003 kuchukua hatua lakini tunapokaribia kufika mwisho utasikia tupeni muda na ukishatoa muda tu wa miezi mitatu au sita ujue ndiyo imetoka.

“Kwahiyo Serikali imeamua kuweka katazo hili kulazimisha mabadiliko ya tabia,” alisema Makamba.

Alisema katazo hilo halikuja kwa kushtukiza kwa sababu  taarifa ya mara ya kwanza ilitolewa bungeni Mei 5, 2016.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kampeni hii kwa sababu suala la mifuko ya plastiki zaidi ni tabia na elimu.

“Kulikuwa na kampeni ya kuonyesha kwamba halifanikiwi, tunaomba mtusaidie, msiingie kwenye mtego huo,” alisema Makamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles