25.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

AFRIKA KUSINI INAPOSHINDWA KUWA MFANO KWA NCHI NYINGINE

NA HILAL K. SUED


Kutokana na historia yake, hususani hali ngumu iliyokuwa ikiwakabili wazalendo wa Kiafrika, namna walivyojikomboa, matumaini makubwa waliyokuwa nayo kutokana na ahadi za viongozi wao, Afrika ya Kusini ilipaswa iwe nchi mfano wa kuigwa na nchi nyingine Barani Afrika zilizojikomboa miongo kadha kabla yake.

Hakuna asiyejua kwamba harakati za ukombozi wa nchi hiyo ulifanyika kwa umwagaji mkubwa wa damu, achilia mbali unyanyasaji, udhalilishaji mkubwa na mateso mengine yasiyoelezeka waliofanyiwa wazalendo katika nchi yao chini ya utawala wa Wazungu wachache.

Isitoshe Afrika ya Kusini ni moja ya nchi duniani zinazopendekezwa na jumuia ya kimataifa kuwa mwanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hivyo kuwa na kura ya Veto kama vile zile nchi tano – Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa na China.

Nchi nyingine zinazopendekezwa katika nafasi hiyo iwapo mabadiliko ndani ya Umoja wa Mataifa yatakubalika ni Brazil, India, na Japan.

Aidha, kufuatana na uimara wa uchumi wake, Afrika ya Kusini ni miongoni mwa kundi la nchi tano liitwalo BRICS (yaani Brazil, Russia, India, China, na South Africa). Nchi hizi, tukiachia Russia, ni zile zinazoendelea na ambazo chumi zake, pamoja na sekta za viwanda na biashara, zimetokea kuimarika kwa kasi katika miongo ya karibuni na hivyo kuwa na ushawishi mkubwa duniani na hususan katika maeneo yao ya jirani.

Kutokana na hali hii, katika Bara la Afrika, Afrika ya Kusini ilikuwa inaonekana kama mfano wa kuigwa na nchi nyingine katika kuchochea maendeleo ya wazalendo wake, uendelezaji wa demokrasia na haki za binadamu.

Kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu kwa mfano, nchi hiyo imepata funzo na/au uzoefu mkubwa kutokana na namna wazalendo wake walivyofanyiwa na watawala wa Wazungu wachache, kama nilivyotamka hapo mbele.

Lakini zaidi ya miongo miwili baada ya kujikomboa, Afrika ya Kusini imeanza kuwa si lolote si chochote, na siyo tu katika masuala ya kujikomboa kiuchumi kwa wazalendo wake, lakini pia katika kukuza na kusimamia haki za binadamu. Imeanza kuwa kama baadhi ya nchi nyingi nyingine Barani humu – kama vile Angola, Nigeria, Equatorial Guinea au Zimbabwe.

Watawala wameanza kuwasahau wazalendo kiuchumi na wao kuanza kujilimbikizia mali kwa njia za kifisadi. Wameanza kuwa kama watawala wa Wazungu wachache waliowang’oa kwa tabu na damu nyingi kumwagika.

Mwezi uliopita ilikuwa madhimisho ya miaka mitano tangu mauaji ya kikatili katika migodi ya Marikana ambako makumi ya wanamgodi waliogoma waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Kuliibuka maswali: Kulikuwa tofauti gani kati ya mauaji ya Sharpeville ya mwaka 1960 au ya Soweto ya mwaka 1976 na ya Marikana? Katika makala yake katika gazeti la The East African, Jenerali Ulimwengu alikwenda mbali zaidi kwa kusema: “Laiti makaburu wangefahamu kwamba wale wazalendo waliokuwa wakipigana nao wangekuja kubadilika na kuwa hivi, wangejiunga nao katika vita vya ukombozi.”

Kwani ni tukio gani ambalo ni la kibaguzi na la kiharamia zaidi kuliko kuwapiga risasi na kuwaua wananchi wasio na silaha za moto, ambao kosa lao kubwa ni kudai mishahara inayokidhi, na halafu yake kuwapeleka mahakamani wale ambao walishindwa kuwauwa na kuwafungulia mashitaka kwa vifo vya wenzao?

Mambo kama haya hayakutarajiwa kabisa kutokea wakati Nelson Mandela anashika nchi mwaka 1994 na hakuna mtu ambaye ameielezea vyema hali hii ya kusikitisha kama Askofu Desmond Tutu.

Tutu alisema kwamba dhana nzima ya wazalendo weusi kujikomboa imepotoshwa, na kinachoonekana sasa ni kama vile waliisimamisha treni yenye uhondo (gravy train) ili nao wapande, na pale anasa zao zinapotishiwa, wale ambao walikuwa wakipigwa risasi hapo zamani ndiyo wenyewe sasa wanatoa amri ya kupiga risasi.

Yaani wapigania uhuru hao badala ya kushughulikia masuala ya kukileta kile walichoahidi kukileta – yaani usawa katika jamii, sasa wameungana na mahasimu wao wa zamani na kuanza kuishi maisha ya anasa kama walivyokuwa wakiishi.

Na ndivyo hali ilivyo, na ndicho kinachopelekea matukio ya Sharpeville na Soweto kuendelezwa na watawala wapya hadi hivi sasa. Ni kama ile riwaya ya George Orwell katika kitabu cha Animal Farm: wanyama katika shamba moja waliung’oa utawala dhalimu (wa mkulima binadamu) na kuanzisha utawala wao kwa matumaini makubwa ya uhuru kamili, haki na usawa, lakini baada ya muda wale watawala waliyongoza ‘mapinduzi’ wakawatupa wenzao na kuanza kuishi maisha ya anasa kama vile yule yule binadamu mkulima dhalimu waliomng’oa.

Kwa maneno mengine watawala sasa wanaanza kuyaona madai ya wazalendo katika kupata sehemu yao stahiki ya keki ya taifa ni tishio kubwa kwao, hadi kufikia hatua ya kuwauwa kwa kuwapiga risasi.

Kama nilivyosema hapo awali, Afrika ya Kusini sasa imekuwa kama nchi nyingine tu Barani Afrika ambazo watawala wamejitenga na umma, wao na maswahiba wao wa kibiashara wakiishi maisha ya anasa kubwa kutokana na ufisadi uliokithiri huku wananchi wengi hawajui jioni watakula nini.

Afrika ya Kusini inaonekana kufuata nyayo za jirani yake Zimbabwe ambayo ilijikomboa kutoka utawala wa kidhalimu wa Wazungu wachache miaka 14 kabla. Miaka michache tu baada ya Zimbabwe kujikomboa baadhi ya mawaziri waandamizi wa serikali ya ZANU-PF walikumbwa na kashfa kubwa iliyojulikana kama Willowgate Scandal walijipa magari ya serikali na baadaye kuyauza kwa faida kubwa.

Nchini Afrika ya Kusini, kuliibuliwa kauli mbiu moja ya kiini macho iliyoitwa “Uwezesho kwa Weusi’ (Black Empowerment) kwa lengo la kuwainua kiuchumi watu weusi baada ya miongo mingi ya utawala wa kidhalimu.

Jacob Zuma, akipigiwa debe na hasimu wake mkubwa wa sasa – Julius Malema, aliweza kuukwaa uongozi wa nchi hiyo baada ya kuondolewa madarakani kwa Thabo Mbeki katikati ya kipindi chake cha pili cha urais baada ya minyukano mikubwa ya kisiasa iliyoanzia pale Mbeki alipomuondoa Zuma kutoka wadhifa wake wa Unaibu wa Rais mwaka 2005.

Hatua hiyo ilitokana na tuhuma za kashfa za ufisadi iliyokuwa ikimkabili akishirikiana na Shabir Shaik, swahiba wake wa kibiashara. Aprili 2009 mamlaka ya uendeshaji wa kesi za jinai zilifuta mashitaka ya ufisadi dhidi yake ingawa swahiba wake huyo alipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela.

Sasa hivi Zuma anakabiliwa na kashfa lukuki za kifisadi na jitihada za kumuondoa kikatiba kupitia Bunge zinashindikana kutokana na uwingi wa Wabunge wa chama chake.

Ni rahisi kuona kwamba nchi hiyo inaendeshwa kwa ghilba kubwa za kisiasa – kawaida ya nchi nyingine nyingi barani humu, wakubwa wakifanya chini juu wasiguswe na mikondo ya sheria pale wanapokumbwa na kashfa za ufisadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles