27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

AfricanLyon inavyojichimbia kaburi yenyewe

Na WINFRIDA MTOI

TIMU ya African Lyon inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa haina kocha mkuu kwa muda mrefu tangu kuondoka kwa Mfaransa, Soccoia Lionel, baada ya kushindwa kuvumilia hali ya ukata klabuni hapo.

Lionel alijiunga na African Lyon msimu huu akiwa pamoja na mshambuliaji wake, Victor da Costa ambaye wameondoka wote.

Kocha huyo aliachana na kikosi hicho raundi ya tisa baada ya mechi yao na Simba kuchapwa mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tangu kuondoka kwa kocha huyo,  kikosi hicho kimekuwa kikiongozwa na meneja wake, Adam Kipatacho, anayesimama kama kocha kwa sasa, akiwa amekaa katika mechi kwa michezo sita.

African Lyon iliyorejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya kushuka, ilikuwa imeanza kuonyesha mwelekeo mzuri chini ya kocha huyo lakini kwa sasa hali inaonekana kwenda tofauti.

 Licha ya kutopata matokeo mazuri katika mechi hizo, Mfaransa huyo alikuwa ametengeneza mfumo ambao angekuwepo hadi kipindi hiki kikosi hicho kingekuwa cha ushindani.

Ukiangalia katika mechi tisa alizocheza,  kufungwa na Stand United bao 1-0, akatoka sare ya bao 1-1 na Alliance, suluhu na Kagera Sugar, michezo yote ya ugenini, kisha kurudi Dar es Salaam na kutoka suluhu na Coastal Union.

Mechi nyingine alikutana na Singida United na kufungwa mabao 3-2, kisha kupoteza kwa Mtibwa Sugar kwa kufungwa mabao 2-0, zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Uhuru.

Baada ya hapo ikatoka tena nje na kwenda kucheza na Ruvu Shooting, wakafungwa bao 1-0 katika Uwanja wa Mabatini, JKT Tanzania bao 1-0, Uwanja wa Meja General Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.

Mfumo wa kocha huyo uliendelea kutumika kwa mafanikio kutokana na wachezaji kuanza kuelewana, lakini hivi sasa unaonekana kuanza kupotea kwani mechi iliyopita walifungwa mabao 4-0 na Mbeya City kabla ya juzi kufungwa na Lipuli FC mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki.

Tofauti na kuondoka kwa kocha huyo, wachezaji wa timu hiyo wameanza kuondoka katika kipindi hiki cha dirisha dogo kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine kutokana na hali mbaya ya kiuchumi.

Ukiangalia wachezaji ambao hawaonekani kambini, asilimia kubwa ni wale wa kikosi cha kwanza waliokuwa wanaibeba timu hiyo kama vile Haruna Moshi ‘Boban’.

Katika msimamo wa ligi, African Lyon ipo nafasi ya 18 ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi 15, ikishinda mbili, sare tano na kupoteza nane.

Kama uongozi wa klabu hiyo hautachukua hatua ya kusaka kocha kwa kipindi hiki, pamoja na kutafuta njia ya kuhakikisha wachezaji wake wanapata mahitaji muhimu na kubaki, itakuwa imejiweka katika mazingira ya kushuka tena.

Tuliona hata msimu wa 2016/2017, kabla haijashuka, African Lyon ilileta kocha  mzungu kutoka Ureno aliyejulikana kwa jina la Bernardo Teveras, naye aliondoka  kabla ya msimu kumalizika.

Licha ya kwamba Teveras aliondoka baada ya kupata timu nyingine, ila kilichochangia ni mwendeno wa timu hiyo hasa katika maslahi kwa wachezaji na benchi la ufundi.

Isingekuwa rahisi kocha huyo kuondoka kama alikuwa akipata maslahi mazuri, hata kama alipata timu nyingine.

Athari za kuondoka kwa Teveras na kuiacha timu aliyoitengeneza ikiwa inaendelea na ligi, ilionekana mwishoni kwani hatimaye mwisho wa msimu huo wa 2016/2017 ilishuka daraja.

Kutokana na hayo, endapo uongozi wa African Lyon utaendelea kuendesha timu kwa ubabaishaji kama huo wa kumpa meneja kikosi, haitashangaza kuona inashuka tena.

Uongozi wa African Lyon haueleweki kama una mapenzi ya dhati na timu hiyo, au wanaiendesha katika misingi ya  kutaka kuonekana na wao wanashiriki  Ligi Kuu.

Mkurugenzi wake, Raheem Kangezi Zamunda, amekuwa mzuri sana katika kutafuta makocha wazungu kushindana na Simba, Yanga na Azam, lakini ameshindwa kutafuta njia ya kuhakikisha kikosi hicho kinasimama.

Fedha anazotumia kuwahangaikia makocha wa kizungu ambao hana uwezo nao ni bora angewapa wazawa  wangemsadia hata katika ushauri.

 Kwa hali ilipofikia kama kweli anahitaji kuona timu hiyo ikisonga mbele, ajaribu kutulia na kuiendesha katika misingi inayotakiwa au kama ameshindwa ni bora awape watu wengine.

Inaonekana wazi kuwa kinachoimaliza African Lyon ni aina ya uongozi uliopo, kwa sababu upande wa wachezaji na benchi la ufundi wamekuwa na bahati ya kuwapata wazuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles