TIMU ya soka ya African Sports jana ilizinduka katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na kuichapa Mbeya City mabao 2-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mabao hayo yaliyofungwa na Omary Ibrahim yaliiwezesha African Sports kufikisha pointi 20 baada ya kucheza michezo 23 huku Mbeya City wakibaki nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi kwa kujikusanyia pointi 24.
Katika mchezo wa jana, African Sports walipoteza nafasi ya kufunga dakika ya 33, baada ya Issa Shaban kushindwa kuunganisha mpira wa krosi iliyochongwa na Ally Ramadhani.
Wenyeji hao walipoteza nafasi nyingine dakika ya 40 baada ya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, James Mendi kushindwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Hassan Materema ambaye alipaisha shuti alilopiga.
African Sports waliandika bao la kwanza dakika ya 56 kupitia kwa Omary aliyefunga kwa shuti alilopiga moja kwa moja kutokana na mpira wa adhabu baada ya Tumba Sued kumchezea faulo Khalfani Twenye.
Omary alifunga bao la pili dakika ya 63 baada ya kumalizia kazi nzuri ya Ally Ramadhani.