Na johns Njozi
Mtandao wa vipindi vya Televisheni wa A+E (A+E Networks), unatarajia kuzindua chaneli mpya ya History itakayokuwa inaonyeshwa katika kisimbuzi cha Azam, Desemba mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja Mkuu wa mtandao huo, Yusuf Nabee, mtandao huo una furaha kuongeza chaneli hiyo baada ya mwaka uliopita kuzindua huduma kadhaa zikiwamo chaneli mbili za Pop-up na H-Vault, huduma ya video kulingana na mahitaji inayowawezesha wateja kuangalia maudhui mbalimbali.
Kwa upande wake Naibu Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa Azam TV, Jacob Joseph, amesema wamefurahi kushirikiana na A+E Networks, kwani Azam inajua mahitaji ya wateja wake na hakika chaneli ya History italeta ladha mpya.
Chaneli ya History itaanza kuonekana kwenye kisimbuzi cha Azam TV, kupitia satelaiti katika chaneli namba 505 na itapatikana kwa wateja walioko Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi na Zimbabwe.