Na TUNU NASSORO-DAR ES SALAAM
CHAMA cha ACT Wazalendo kimeainisha maeneo ya kipaumbele ambayo itakuwa ndiyo dira yake kwa mwaka huu mpya 2018.
Vipaumbele hivyo ni pamoja na uchaguzi wa ngazi zote kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho na misingi ya kidemokrasia.
Akitoa mwelekeo huo kwa vyombo vya habari jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema Kilele cha uchaguzi kitakuwa mwezi Agosti, 2018 mkutano mkuu kama chombo cha juu zaidi cha maamuzi chenye uwakilishi kutoka kila jimbo utafanyika Jijini Mbeya na kuchagua viongozi wa juu wakiwamo Kiongozi wa chama, Mwenyekiti na Makamu wenyeviti.
“Tunatoa wito kwa wanachama wote katika ngazi mbalimbali kujitokeza kugombea. Mkutano Mkuu utatanguliwa na Mkutano Mkuu wa kidemokrasia ambalo ni jukwaa la chama linalotumika kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa”alisema
Aidha Shaibu alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kuimarisha ushirikiano na wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi.
Alisema Kamati Kuu iliazimia kuimarisha ushiriki wa chama chao kwenye mapambano ya wafanyakazi kwa kutambua kwamba wafanyakazi, serikalini na kwenye sekta binafsi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo za mishahara na mazingira duni ya kazi na vitendo pamoja na mbalimbali vya uonevu vinavyofanywa na waajiri wao.
Katika mwelekeo huo, Shaibu alisema ACT wazalendo kitaongeza maradufu ushirikiano na vyama vingine vya upinzani kwenye mapambano ya kupigania demokrasia na Katiba mpya.
“Jambo hili linasukumwa na ukweli kwamba Serikali imejipambanua bila soni kuwa hodari katika kuivunja misingi ya demokrasia nchini. Vita ya kuitetea na kuilinda misingi ya kidemokrasia haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano madhubuti baina ya vyama vya upinzani na wananchi kwa ujumla,”alisema