Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kuharakisha uundwaji wa tume huru ya uchaguzi itakayosimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza Aprili 8,2024 na Waandishi wa habari Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita, amesema moja ya wajibu wa tume ni kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa hivyo maandalizi yake yanapaswa kuanza sasa.
Mchinjita alikuwa akichambua hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuhusu bajeti na mwelekeo wa Serikali kwa mwaka 2024/25.
“Serikali ipeleke muswada wa sheria ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika Bunge linaloendelea sasa ili kuhakikisha unasimamiwa na tume na si Tamisemi…ACT Wazalendo hatupo tayari kwenda kwenye uchaguzi utakaosimamiwa na Tamisemi,” amesema Mchinjita.
Chama hicho pia kimeitaka Serikali kutenga bajeti ya kutosha ili kujenga uwezo wa idara ya maafa na kuongeza ufanisi wa usimamizi wa idara hiyo.
“Tunamtaka Waziri Mkuu afike Rufiji na Kibiti kuona hali halisi na kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa kwa wananchi wa maeneo hayo ambayo kwa sasa ni hatarishi na walipwe fidia. Afike pia Mlimba kujionea hali halisi na kuchukua hatua stahiki,” amesema.
Kwa mujibu wa Mchinjita, kata 12 zilizoko ukanda wa Kibiti na Rufiji eneo linalozunguka Bonde la Mto Rufiji lililopo karibu na Bwawa la Mwalimu Nyerere zimeathiriwa na mafuriko na kusababisha makazi na mazao kuharibika.
Amesema pia Kijiji cha Taweta Kilombero mawasiliano bado hayajarudi na zaidi ya watu 1,000 wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu.
Maeneo mengine ambayo chama hicho kimedai hayajapatiwa ufumbuzi kutokana na hotuba hiyo ni suala la hali ngumu ya maisha kulikochangiwa na kupanda kwa bei za vyakula, mafuta ya petroli, dizeli na taa pamoja na bidhaa za ujenzi.
Chama hicho kimeishauri Serikali kuiongezea uwezo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili uweze kununua chakula cha kutosha kujilinda na upungufu na kupaa kwa bei.
“Serikali iweke zuio kwa wazalishaji wa saruji kuagiza malighafi nje zinazopatikana nchini ili kuacha faida ndani, kukuza ajira na kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu,” amesema Mchinjita.
Maeneo mengine ni ruzuku ya uendeshaji wa shule, suala la ukosefu wa ajira na masilahi ya wafanyakazi hasa kikokotoo cha mafao ambacho wafanyakazi wengi wanalalamikia kanuni mpya zilizoanzwa kutekelezwa Julai 2023.