CALIFORNIA, MAREKANI
MTANDAO wa Twitter umezindua huduma mpya inayoitwa ‘fleets’, tweets ambazo hupotea baada ya saa 24, sawa na machapisho kwenye Snapchat na Instagram.
Twitter hapo awali ilitangaza mpango wake wa tweets hizi za muda, zilizopewa jina la ‘fleet’, na kufanyia majaribio huduma hiyo huko Brazil, Italia, India na Korea Kusini.
“Baadhi yenu mnatuambia kuwa kutumia twitter ni wasiwasi kwa sababu inahisiwa kuwa ni kujianika zaidi, ni ya kudumu, na vile kuna shinikizo kubwa la kusisitiza ujumbe uliopendwa kwa kuuchapisha tena (retweet) na kupenda (like),” Mkurugenzi wa ubunifu wa Twitter, Joshua Harris, na meneja bidhaa, Sam Haveson, waliandika katika chapisho la blog.
“Kwakuwa ujumbe unatoweka baada ya siku moja, hatua hii itawasaidia watu kujiamini kuweka taarifa na mawazo yao pia hisia zao.”
Baadhi ya watumiaji wa Twitter waliokuwa wakifanyia majaribio huduma hii wamesema mtandao huo ulikuwa unasababisha wasiwasi wa uwezekano wa kudhalilishwa mtandaoni, kwa kuruhusu ujumbe wa moja kwa moja usiohitajika. Pia ujumbe kuwafikia watu uliowafungia kupata taarifa.
Twitter imesema ilikuwa ikipokea mrejesho na kufanyia kazi masuala yanayogusa usalama wa watumiaji wa mtandao huo.
‘Fleets’ zinaweza kujumuisha maandishi, picha na video. Vitapatikana kwa watumiaji kwenye mfululizo wa matukio ya picha, maandishi na video za matukio (timelines) kwenye Twitter na maelezo kuhusu mtumaji (profile).
Twitter na kampuni nyingine za mitandao ya kijamii ziko kwenye shinikizo kubwa kudhibiti matumizi mabaya na upotoshaji wa taarifa unaosambaa.
Msemaji wa Twitter, Liz Kelley alisema ‘fleets’ zitakuwa na masharti yale yale kama ilivyo kwa machapisho ya kuwekwa twitter.
Kelley alisema kuwa tahadhari ambazo wameanza kuziweka kwenye maudhui kama vile taarifa za uongo na taarifa potofu kwa mfano Covid-19 zinaweza pia kuwekwa kwenye ‘fleet’.
Twitter imethibitisha kuwa ilikuwa ikifanyia kazi sauti zinazoingia moja kwa moja, ziitwazo Spaces, ambayo itafanyiwa majaribio hivi karibuni.
Spaces itaruhusu watumiaji kufanya mazungumzo wakiwa kwenye kikundi. Inafanana na Clubhouse, jukwaa linalotumia mazungumzo ya sauti kwenye kikundi.
Awali mwaka huu Twitter ilianzisha mfumo wa watumiaji kuchapisha sauti kwenye mtandao huo.