33.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Ndege ya Tanzania yavinjari Somalia

Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, akishuka kwenye ndege ya ATCL mjini Mogadishu, Somalia, juzi
Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, akishuka kwenye ndege ya ATCL mjini Mogadishu, Somalia, juzi

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

NDEGE ya Tanzania inayomilikiwa na Shirika la Ndege la ATCL, imetua nchini Somalia huku hofu ikitawala kuhusu usalama wake.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka ATCL, ndege hiyo aina ya CRJ Bomber-200, ilimbeba Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, huku uongozi wa shirika hilo ukiwa haujui namna ilivyofika nchini humo.

Chanzo hicho kiliiambia MTANZANIA kuwa ndege hiyo hupelekwa nchini Kenya kwa ajili ya matengenezo ya kawaida na kurejea nchini kwa mujibu wa utaratibu.

Rais Mohamud alikuwa nchini Marekani katika mkutano wa Rais Barack Obama na marais kutoka nchi za Afrika.

“Baada ya Rais Mohamud kutoka nchini Marekani, alitua jijini Nairobi jana (juzi), na baada ya muda alibebwa na ndege yenye nembo ya ATCL na kupelekwa nchini Somalia.

“Sio siri, hofu ilitawala sana na hata kujiuliza kama itafika na kurudi salama kutokana na tishio la Al-Shabaab ambao kwa muda sasa wamekuwa wakifanya vitendo vya kigaidi katika nchi za Afrika Mashariki, ikiwamo hata kuwa na mawakala wao katika nchi kadhaa,” alisema mtoa habari huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini.

Kutokana na hali hiyo ya machafuko nchini Somalia, baadhi ya watu walishangazwa kufika salama kwa ndege hiyo licha ya kuwapo kwa mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wanamgambo wa Kiislamu wa Al-Shabaab.

Hatua ya ndege hiyo kutua nchini humo, iliwashangaza wananchi wa Somalia ambao kwa miaka kadhaa wamezoea kuona ndege zenye nembo ya Umoja wa Mataifa zikipeleka misaada ya dharura, hasa dawa na chakula.

Somalia imekuwa ikikumbwa na machafuko ya mara kwa mara ikiwamo tukio la Septemba 13, mwaka juzi ambapo Rais Mohamud alinusurika katika jaribio la kumuua mjini Mogadishu.

Milipuko miwili ilitokea nje ya lango la makao yake katika hoteli ya Al-Jazeera wakati alipokuwa anafanya mkutano na waandishi wa habari.

Kauli ya ATCL

Akizungumzia sakata hilo jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Kapteni Milton Lazaro, alishangazwa na hatua ya ndege hiyo iliyokuwa katika matengenezo kuonekana Somalia ikiwa imemebeba rais wa nchi hiyo bila taarifa zozote.

Kapteni Lazaro, alisema ndege hiyo ya kukodi hivi sasa ipo kwenye mikono ya ATCL na hukaa baada ya muda na kwenda nchini Kenya kwa ajili ya matengezo ya kawaida.

“Hata sisi tunashangazwa na hizi taarifa za ndege hii ambayo ilikwenda ‘check up’ ya kawaida Nairobi, sasa tunatafuta taarifa za kina inakuwaje iende Mogadishu bila taarifa,” alisema Kapteni Lazaro.

Julai 10, mwaka huu, Rais Mohamud alitangaza kuwafuta kazi wakuu wa Jeshi la Polisi na Idara ya Upelelezi ya nchi hiyo kutokana na shambulizi lililofanywa na wanamgambo wa Al-Shabaab dhidi ya Ikulu ya Rais mjini Mogadishu.

Rais huyo wa Somalia alimteua mkuu wa zamani wa upelelezi, Khalif Ahmed Ereg, kuwa Waziri mpya wa Usalama wa Taifa.

Mabadiliko hayo yamefanyika baada ya wapiganaji wa Al-Shabaab kushambulia Ikulu Julai 8, mwaka huu ambapo watu kadhaa waliuawa.

Mashambulizi hayo dhidi ya Ikulu mjini Mogadishu si ya kwanza kufanywa na wapiganaji hao.

Mwezi Februari mwaka huu wapiganaji wa Al-Shabaab waliokuwa na sare za jeshi, walishambulia Ikulu hiyo wakiwa na gari lililokuwa na mabomu. Wote waliuawa.

Mei mwaka huu, walishambulia jengo la Bunge wakati wabunge walipokuwa katika kikao ambapo walinzi na maofisa kadhaa waliuawa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles