26.3 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa asema CCM haitaaacha nyuma wajasiriamali

Na Mwandishi wetu, Kahama

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ijayo ya chama chake itaendelea kuwaunga mkono na kuwaendeleza wajasiriamali wakiwemo wasanii.

Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Kahama katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Magufuli mjini Kahama, mkoani Shinyanga. 

“Serikali ya CCM inawathamini sana wasanii kwa sababu sanaa ni sawa na ujasiriamali. Kwa maana hiyo, sanaa ni ajira,” alisema.

Akielezea kuhusu ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa, Majaliwa alisema kwenye ilani ya uchaguzi, barabara kubwa inayotajwa kuunganisha mji wa Kahama na mikoa ya jirani ni ya kutoka Katavi hadi Tabora kupitia Ugalla.

“Katika uk. 73, Ilani yetu inataja barabara zinatotakiwa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambazo ni Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyankulu – Kahama (km 428); Geita – Bukoli – Kahama (km 107) na Kahama – Nyamilangano – Uyogo (km 54).”

Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake ya kumuombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli alimnadi pia mgombea ubunge wa Jimbo la Kahama mjini, Jumanne Kishimba na wagombea udiwani wa wilaya hiyo. 

Katika hatua nyingine, Waziri wa Madini, Dotto Biteko alisema Wilaya ya Kahama imepanda chati ya makusanyo yatokanayo na madini kutokana na usimamizi wa Serikali ya awamu ya tano.

“Kwenye makusanyo ya madini, Kahama ilikuwa ikishika nafasi ya nne. Sasa hivi imepanda na kuchukua nafasi ya pili. Mnashindana na Geita. Chunya ndiyo ilikuwa ikishika nafasi ya pili lakini sasa hivi mmeiacha mbali. Chagueni viongozi wa CCM ili iendelee kuwaletea neema,” alisema.

Akiwa Isaka, wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga aliwataka wananchi wa eneo hilo wawe tayari kutumia fursa ya ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa bandari kavu ili kujiletea maendeleo.

 “Kwanza kutakuwa na bandari kavu ambayo itakuwa inapokea mizigo kutoka nchi tofauti zinazotuzunguka. Kwa hiyo wana Kagongwa, tumieni fursa hii kufanya biashara. Wana Isaka tumieni fursa hii kujenga nyumba za kulala wageni na mahoteli ya kuuza vyakula.

“Pili ni reli ya kisasa ambayo tunapanga kuijenga itapita hapa Isaka. Reli hii ikikamilika, mtu atakuwa anatumia saa nne kwenda Dar es Salaam badala ya saa 14 ambazo zinatumika hivi sasa kwa usafiri wa mabasi.”

Akizungumza na wakazi wa Kata za Segese na Kakola, Majaliwa alisema barabara ya kutoka Geita kupitia Kagongo hadi Kahama yenye urefu wa KM 106 itajengwa kwa kiwango cha lami.

“Barabara hii ilikuwemo kwenye ilani inayomalizika sasa uk.66 na ilipangiwa kufanyiwa upembuzi yakinifu lakini katika ilani yetu ya sasa, inatakiwa kukamilishwa ili wananchi muanze kufanya biashara kwa urahisi.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles