CHAMA cha kutetea haki za wasanii wa muziki wa kizazi kipya (TUMA) kimeeleza kwamba wasanii wengi wa muziki huo wanakosa haki zao kwa kuwa si wanachama wa chama hicho.
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Samweli Briton, alisema ingawa kwa sasa baadhi ya wasanii wametambua hilo, lakini idadi ya wanaojitokeza inabidi iongezeke ili chama hicho kiwe na wanachama wengi kitakachoongeza nguvu katika utetezi wake.
“Wasanii zaidi ya 30 wameshachukua fomu za kujiunga na chama hicho, akiwemo Vanessa Mdee, Barnaba Boy, Wakazi, Ditto na wengine wengi, hivyo natoa wito kwa wasanii wengine chipukizi na wenye majina kujiunga na chama hiki kabla ya kusubiri matatizo katika kazi zao,’’ alieleza Briton.
Hata hivyo, mmoja wa wasanii hao, Wakazi alisema amekuwa daraja la kuwashawishi wasanii wa muziki huo ili wajiunge na chama hicho wanachoamini kitawasaidia katika harakati zao za kupata mirabaha itakayotokana na kazi zao.