FARAJA MASINDE na JULIANA SAMWELY (TUDARCo) – DAR ES SALAAM
MTUNZI Mahiri wa Vitabu vya Tamthilia nchini, Majdi Mswahili, amezindua kitabu ambacho mbali na mambo mengine kinampongeza Rais Dk. John Magfuli kwa namna alivyo pambana na janga la virusi vya corona.
Akizungumzia kitabu hicho alichokipa jina la ‘Kizungumkuti’alichokizindua juzi katika hafla fupi iliyofanyika kwenye duka la kuuzia vitabu la Elite Book, lililoko Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.
Mswahili alisema kuwa Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa ambayo yameifanya Tanzania kuwa ya kipekee ikiwamo janga la corona, jambo ambalo lilimsukuma kuandika kitabu hicho ambazho anatamani kimfikie.
“Pamoja na viongozi wote waliotangulia kuliongoza taifa letu kufanya mambo mazuri, lakini Dk. Magufuli ametufanya tuendelee na maisha yetu na kutuondoa hofu, uthubutu ambao umetufanya tuendelee na maisha yetu na kuishangaza dunia katika janga hili la corona, hivyo kuna kila sababu ya kumpongeza rais wetu.
“Kwani mara hii ulivyotokea ugonjwa wa virusi vya corona tulilazimika kukaa ndani, jambo ambalo lilibadilisha mfumo wetu wa maisha. Hatari zaidi ilikuwa ni namna vyombo vya habari vya nje vilivyokuwa vikiripoti kuhusu virusi hivyo nchini na hali halisi jambo ambalo lilinifanya niandike ‘Kizungumkuti’kwani watu kama yeye na wenye uthubutu kama wake hawapatikani kirahisi sana.
“Hivyo nimeandika kitabu hiki ili aone kwamba nchi yake bado ina vijana wazuri wanaweza kukaa chini na kuchambua mazuri yaliyoko nchini,” alisema Mswahili.
Alisema kuwa kitabu hicho chenye kauli mbiu ya ‘Soma useme’ kina manufaa kwa kila mtanzania nakwamba mbali na kutamani kimfike rais Magufuli pia anatamani watanzania wengi zaidi kukisoma huku akiwakumbusha watunzi wengine kuwa soko la vitabu lipo na wanaweza kupata mafanikio.
“Ninacho waomba watunzi wenzangu, tuendelee kufanya kazi nzuri kwa kushirikiana na walezi wetu ambao ni Baraza la Kiswahili la Taifa(BAKITA), ili kukuza tasnia ya utunzi nchini, kwani lipo kwa ajili yetu hivyo tunapaswa kushirikiana nao hata kama hatuna fedha,”alisema Mswahili.
Upande wake, Mshiriki wa Taaluma ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa, Adrian Mtembei akizungumzia kitabu hicho alipongeza kwa namna ambavyo kimetumia mfumo wa kisasa wa Sayansi na Teknolojia katika uandaaji wake.
“Hii ni tamthilia nzuri ambayo mtindo wake ni wakipekee kuanzia teknolojia ya undaaji, pia wametumia wahusika wasio wa kawaida kama moyo na mapafu na kuifanya tamthilia hii kuwa ya kipekee,” alisema Prof. Mtembei.