30.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

Chadema yailalamikia NEC kutojibu rufaa za wagombea

Na MWANDISHI WETU–DAR ES SALAAM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kutotoa majibu ya rufaa za wagombea ubunge 16 na za udiwani zaidi ya 300.

Kutokana na hilo, kimesema tayari kimeiandikia barua tume hiyo, ikitaka muafaka juu ya majibu ya rufaa za wagombea wake walioenguliwa ‘kinyume’ cha sheria.

Hayo yalisemwa  na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

“Tangu Agosti 28, mwaka huu, tume imekuwa ikipokea rufaa za wagombea wetu wa ubunge na udiwani waliokuwa wameenguliwa baada ya mapingamizi. 

“Tume imepokea rufaa, safari  hii nadhani imevunja rekodi haijapata kutokea kwa sababu mwaka 2015 rufaa za udiwani hazikuzidi 71, ubunge zilikuwa 11 nchini nzima.

“Mara hii rufaa ziko mamia na zikaribia maelfu. Chadema peke yetu tulipeleka rufaa za ubunge zaidi ya 49 malalamiko kwa maana ya wale ambao hawakupewa fomu za rufaa na za udiwani zilikuwa zaidi ya 600.

“Hadi sasa rufaa za wagombea 16 wa ubunge wa Chadema hazijatolewa uamuzi na za udiwani ni zaidi ya 300, zimebaki siku 35 watu wapige kura.

“Tayari tumeiandikia barua tume kuhusu  wasimamizi wao  wanaovunja sheria ili wasiendelee kubariki, hatutaruhusu sheria zivunjwe na kanuni zikiukwe kwa sababu ya kuwapendelea wagombea wa vyama fulani,”alisema.

Mgombea ubunge kupitia chama hicho katika Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Susan Kiwanga ambaye ni miongoni mwa wagombea ambao hawajapata majibu ya rufaa zao, aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano huo kuwa tume iwape haki yao kwa kuwapa majibu ya rufaa zao.

 “Mlimba hali ni tete, naogopa kukaa kule kwa sababu nikikaa kule watajua nawashawishi wananchi kufanya fujo. Kule hali ni tete, wanataka kujua hatima yao.

“Tunaitaka tume watoe majibu ya rufaa zetu, watoe iwe mabaya au yawe mazuri. Tunateseka ni haki yetu kupata majibu ya tume na si vinginevyo,”alisema Kiwanga.

Naye mgombea ubunge Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Onesmo Francis Mbuya aliiomba NEC itoe majibu ya rufaa zao ili wagombea waendelee na mchakato wa uchaguzi.

“Morogoro Kusini Mashariki kuna msiba, watu wamepigwa na butwaa kwa sababu wanajua hawatafanya uchaguzi wa mbunge, mgombea wa CCM anajisifu amepita bila kupingwa. 

“Jimbo langu lina kata 14 kati ya hizo mbili tu wagombea wake wameteuliwa, wagombea 12 hali kama yangu wamekata rufaa hadi leo NEC hawajajibu kwa barua,”alisema Mbuya.

Aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufanya uchunguzi katika maeneo ya uchaguzi ambayo wagombea wake wamepita bila kupingwa, kwa madai kwamba kuna viashiria vya vitendo vya rushwa.

“Takukuru wapite katika maeneo ya majimbo ambayo wagombea wamepita bila kupingwa, kwa sababu kuna vimelea vya rushwa. Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki baada ya mgombea kutangazwa kupita bila kupingwa, walifanya sherehe ya kula chakula cha mchana ambacho wamenunuliwa na mgombea aliyetangazwa bila kupingwa,”alisema Mbuya .

Mgombea ubunge Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, James Haule alisema katika jimbo lake yeye pamoja na wagombea udiwani 14 wamekatwa na hadi leo majibu yao ya rufaa hawajapewa.

“Uchaguzi huu umekuwa ni kituko. Wananchi wa Ludewa wanalalamika wamekatwa madiwa 14 lengo tusiendeshe halmashauri. 

“Tunaitaka tume kurejesha wagombea udiwani Halmashauri ya Ludewa bila masharti, tunahitaji haki itendeke kwa wananchi ndio kazi ya tume,”alisema Haule.

Mgombea ubunge Jimbo la Nzega Vijijni mkoani Tabora, Monica Nsalo naye aliiomba tume  impe majibu ya barua ya rufaa yake, kuhusu pingamizi aliyowekewa na mgombea wa Chama Cha Mapindiz (CCM), Dk. Hamis Kigwangallah aliyetangazwa amepita bila kupingwa.

“Sijapewa majibu ya rufaa zangu, hadi leo inaendelea kutangazwa Kigwangalla amepita bila kupingwa licha ya kwamba rufaa zangu hazijatolewa majibu.

“Tunahitaji kusimama tufanye kampeni sio tume ibebe watu na wengine iwaonee. Mimi ni mwanamke kwanini tume inashindwa kurudisha jina langu tukafanye kampeni ili tushindane kwenye sanduku la kura,”alihoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,507FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles