24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Viongozi, wachezaji timizeni wajibu wenu

MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unazidi kushuka kasi.

Msimu huu, ligi hiyo inashirikisha timu 18 badala ya 20 zilizochuana msimu uliopita na kushuhudiwa  Simba ikitwaa ubingwa.

Kila timu imejitahidi kufanya usajili  kadri ya uwezo wake, lengo likiwa kuboresha kasoro zilizoonekana msimu uliopita, lakini pia kuziba nafasi zilizoachwa na wachezaji waliohamia timu nyingine au kuachwa kutokana na kushuka viwango.

Zipo timu zilizosajili wachezaji wa kigeni mbali ya wale wa ndani.

Haya yote yamefanyika kwa kusudio la kuhakikisha zinafanya vizuri msimu ujao.

MTANZANIA  tunazitakila kila la heri timu zote 18 zitakazoshiriki ligi hiyo msumu ujao.

Ni matumaini yetu, usajili wa mbwembwe tulioushuhudia utahamishiwa uwanjani kwa timu kuonyesha ushindani ambao ndio hasa wapenzi wa soka wanatarajia kuuona.

Tukiwa wadau wa michezo ukiwemo soka hatutarajii kuona timu ikisaka matokeo kwa njia zisizo halali, badala yake yule aliyejiandaa kikamilifu ndio apate haki yake ya kupata ushindi.

Ni matarajio yetu ushindani tulioushuhudia msimu uliopita, safari hii utakuwa mkubwa zaidi.

Hili likifanikiwa maana yake litaongeza ubora wa ligi yetu, hatua itakayoiwezesha pia kujitangaza na kuwa maarufu zaidi barani Afrika kama sio duniani.

Ligi ikiwa maarufu na yenye ushindani, itasaidia kuwavutia wadhamini wengi zaidi kujitokeza kuwekeza fedha zao wakiamini itakuwa inafatiliwa zaidi.

Lakini pia udhamini ukiongezea maana yake ni kwamba, hali ya uchumi za klabu zitakuwa nzuri zaidi tofauti na sasa ambapo ni baadhi tu ndizo zimekuwa zikimudu kutimiza  mambo ya msingi kama kulipa mishahara  kwa wafanyakazi na wachezaji wao.

Kwa upande wa mchezaji mmoja mmoja, tunatarajia mtazipigania timu zetu ili ziweze kufikia malengo, ukizingatia zimetumia fedha katika kufanya maboresho  ambayo ni pamoja na kufanya usajili wa wachezaji wapya.

Kila mchezaji aone kwamba amesajiliwa kwa ajili ya kucheza na sio kusugua benchi, hivyo ahakikishe anapambana kuhakikisha anapata nafasi ya kucheza.

Hii itakuwa si tu faida kwa timu bali pia kwa mchezaji kwani itamwezesha kulinda na kukuza kipaji chake.

Pia ni imani yetu viongozi wa klabu mbalimbali zitakazoshiriki ligi hiyo watahakikisha wanatimiza mahitaji ya msingi ya wachezaji na kuepuka ubabaishaji ambao umekuwa ukishuhudiwa huko nyuma.

Ni muhimu kuhakikisha wachezaji wanalipwa stahiki zao kwa wakati ikiwemo mishahara  kulingana na makubaliano ya kwenye mikataba.

Hili likifanyika litasaidia kuwafanya wachezaji waelekeza akili zao  uwanjani na kuzitumia timu zao kwa moyo wao wote hivyo kuongeza ushindani katika ligi, kitu ambacho sisi wadau wa soka tunakihitaji.

Tuliona msimu uliopita baadhi ya wachezaji walilalamika kutolipwa stahiki zao kwa wakati kiasi kwamba wapo waliofikia uamuzi wa kugoma kutumika.

Lakini pia ligi hiyo ikiwa na ushindani itasaidia kupatikana kwa wachezaji bora ambao watatumika pia kuunda timu imara ya Taifa ambayo itashiriki michuano mbalimbali ya kimataifa na kufanya vizuri. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles