NORA DAMIAN Na MWANDISHI WETU -GEITA/DAR
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema siku kumi za kampeni zimekuwa na mafanikio kwani mwaka huu zinafanyika kisayansi na kwa kuzingatia weledi wa hali ya juu.
Aidha kimesema kwa siku 10 ambazo mgombea urais, Dk. John Magufuli amefanya kampeni iwapo uchaguzi ungefanyika sasa angeshinda kwa zaidi ya asilimia 85.
Wakati CCM ikitoa tathimini hiyo jana, mapema wiki hii mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari alisema anaona katika uchaguzi huu wanaweza kushinda kwa kiasi kikubwa na hata kuiangusha CCM madarakani.
Zaidi chama hicho cha upinzani kama ilivyo kwa CCM, kinaonekana kuchora upya ramani ya kufanya kampeni kwa vigogo wake kusambaa katika kanda mbalimbali za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema katika kampeni hizo wamejikita kueleza mageuzi makubwa ya kiuchumi yaliyofanywa na Dk. Magufuli na yale yatakayofanywa kwa miaka mitano ijayo.
“Kampeni kwa ujumla zinakwenda vizuri na kampeni zetu ni rahisi mno kwa sababu tuna utajiri wa kazi nzuri tunazofanya tunawaeleza umma wa Watanzania.
“Tunaeleza kwanini tunahitaji kumalizia tena kazi hii pamoja, tunakutana na Watanzania na kuwaeleza mafanikio. Watanzania wametuamini, wanatuheshimu, wanatupenda.
“Tumeamua kujikita kwenye ‘facts and figures’, tunajikita kufafanua tulipotoka, tulipo na tunapoelekea. Siku kumi za kampeni kwa kazi nzuri ambayo imefanyika umma umetuelewa, kimsingi nchi tumeishika na kila tunapofika Watanzania wanatuelewa,” alisema Polepole.
Alisema walifanya utafiti na kugundua kuwa Watanzania wanapenda kusikiliza sera ndiyo maana maeneo mbalimbali waliyokwenda walipata mapokezi makubwa.
KAMPENI ZINAVYOFANYIKA
Polepole alisema licha ya kampeni za Dk. Magufuli pia wapo makada waandamizi na viongozi mbalimbali ambao nao wanaendelea na kampeni kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.
“Tumejenga taasisi imara yenye makada madhubuti, tuna makada waandamizi na viongozi katika maeneo mbalimbali ya nchi, Dk. Magufuli ameshambulia maeneo mbalimbali amekutana na mamilioni ya Watanzania ambao wamemlaki.
“Mgombea mwenza naye amechukua maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa amechukua maeneo ya Dodoma, Manyara, Kilimanjaro na Arusha.
“Mwenyekiti na rais mstaafu, Jakaya Kikwete anashambulia…kampeni ni sayansi, kampeni ni mkakati mahali ambapo kuna watu wavurugaji unapeleka mtu ambaye anafahamu zaidi,” alisema Polepole.
Kwa mujibu wa Polepole wakongwe wengine ndani ya chama hicho ambao wanaendelea na kampeni ya kunadi sera na kukiombea kura chama ni pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda na Spika wa Bunge, Job Ndugai ambao wanashambulia Kanda ya Kati.
“Tuko vizuri sana tumesambaa Tanzania na sasa hivi tumefanya tathmini tunakwenda tena awamu ya pili…hadi tarehe 27 (siku moja kabla ya kupiga kura) tutakuwa tumefika kijiji kwa kijiji, barabara kwa barabara, wilaya kwa wilaya.
“Msingi wa kampeni uko wilayani, majimbo na kwenye kata na kuna makada wengi, wako wabunge waliopita bila kupingwa wataendelea kushambulia kueleza mazuri yaliyofanyika katika nchi hii na kueleza maono ya chama,” alisema.
MTAJI WA KURA
Polepole alisema wanacho kitengo cha utafiti ambacho kimekuwa kikishirikiana na wadau mbalimbali wa utafiti kufanya tafiti za kisayansi na zenye weledi unaopimwa kwa vigezo vya kimataifa.
“Tumekuwa tukifanya tafiti za kisayansi mara kwa mara na ndani ya siku kumi tulizofanya kampeni tumegundua kama kura ingepigwa leo Dk. Magufuli angeshinda kwa zaidi ya asilimia 85,” alisema Polepole.
Alisema pia wanao mtaji mwingine wa wanachama milioni 17 na kwamba kwa idadi hiyo tu tayari wana ushindi wa zaidi ya asilimia 60.
Alisema hata katika maeneo ambayo hayana wawakilishi wa CCM wana imani watashinda kwa kishindo kwa sababu walipeleka maendeleo kwa usawa.
“Mfano Arusha tulipoteza kabisa, udiwani tulikuwa na kata moja tu lakini katika mkoa ambao ulipokea fedha nyingi za maendeleo ni Arusha. Bilioni 500 zimeingia pale, mkakati wetu ulikuwa kuwapatia maendeleo bila ubaguzi,” alisema Polepole.
UMOJA WA KITAIFA
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliviasa vyama vya siasa kuepuka kupotosha umma na badala yake vifanye kampeni za kistaarabu ili kuendelea kujenga umoja wa kitaifa.
Alisema wao wanataka wawe mfano kwa kufanya kampeni safi na za kistaarabu zinazozingatia weledi, sheria na maadili pamoja na kanuni za uchaguzi.
“Baadhi ya vyama vinatoa kauli ambazo hazijengi umoja wa nchi yetu, kauli zinazoathiri uhuru na maisha ya watu, kauli zinazoondoa umoja wa kitaifa.
“Tunalaani vitendo vinavyokosa utu, ustahimilivu wa kisiasa na vinavyovunja sheria na kanuni, siasa za ujanja ujanja na visingizio hazina mashiko.
“Unapokuwa kiongozi hata kama ni chama cha upinzani bado unawajibika kusimama pamoja katika mambo ya kitaifa, siasa dhaifu hazitupeleki mahali popote…Watanzania wanataka kusikiliza sera na mambo yanayohusu maisha yao,” alisema Polepole.
AFAFANUA MIRADI INAYOENDELEA GEITA
Polepole alisema baadhi ya miradi inayoendelea mkoani Geita ipo pia katika mikoa mingine na kuwataka Watanzania kupuuza upotoshaji unaoendelea.
“Geita ni mkoa mpya hauna ‘airport’ tumenunua ndege nyingi ziwahudumie Watanzania wa mikoa yote, zitoe huduma kote na tumesema tutatandaza viwanja vya ndege na Geita ni mojawapo.
“Uwanja wa ndege Mwanza ni mkubwa kuliko wowote katika Ukanda wa Maziwa Makuu, lazima kuwe na uwanja mwingine wa kimkakati ikitokea dharura wasilazimike kwenda Dar es Salaam, Kilimanjaro, Burundi ni mbali hivyo, eneo ambalo limewekwa kimkakati ni Geita na hivi viwanja viko kila mahali.
“Kulikuwa na pori haliingizi fedha lakini ukifanya mbuga za wanyama watalii wanakuja tunapata fedha…watu kama hawa wapuuzwe kwani Watanzania wanajua ukweli wa kazi ambayo imeshafanyika,” alisema Polepole.
RUFAA ZA NEC
Akizungumzia uamuzi wa rufaa uliotolewa hivi karibuni na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambao uliwarejesha baadhi ya wagombea ubunge ambao awali walitangazwa kupita bila kupingwa, Polepole alisema; “ Iwe isiwe tutawachapa.
KUHUSU ZANZIBAR
Polepole alisema; “Kule kazi imeshakwisha, Wazanzibar wanatuelewa, wanapenda kuona damu changa, mtu ambaye amedumu kwenye uongozi,” alisema Polepole.